Habari Mseto

Wachina waliokuwa Kenya waruhusiwa kurudi kwao

June 17th, 2020 1 min read

STEVE NJUGUNA

Serikali ya China itawatoa wananchi wake 400 kutoka Kenya, huku kikundi cha kwanza kikiondoka Jumanne saa tano usiku kwa kuhofia virusi vya corona.

Wachina hao walichukua tiketi zao Jumapili lakini hawangeweza kutoshea kwa ndege moja ya China Southern Airline kutokana na kanuni ya kuweka umbali wa mita moja.

“Waliobaki 200 tunajarajia warudi China wiki hii. Tulitarajia wangesafiri wote lakini haikuwezekana kwa sababu ya kanuni mpya ya usafiri ya umbali wa mita moja,” alisema Isaac Okinyo.

Mipango ya mwisho ya kuwatoa Wachina hao ilifanyika baada ya Wizara ya Maswala ya Kigeni kuwapa ruhusa ya kuwatoa humu nchini.

Bw Isaac Okinyo aliambia Taifa Leo kwamba Wachina hao walikuwa wameomba ruhusa ya kutoka humu nchini kwa wizara hiyo lakini ubalozi wa Uchina ukakataa.

Hii ilimlazimu kwenda kortini ambapo serikali ya Kenya iliagizwa kuwaruhusu waondoke Juni 16, kwa sababu Wizara ya Afya ya Kenya imelemewa kukabiliana na corona.

Jaji alitoa amri baada ya mwanasheria huyo kuomba ruhusa ya kipekee ya kuwatoa Wachina hao humu nchini.

Mwanasheria huyo aliwasilisha agizo hilo la korti kwa Wizara ya Masuala ya Kigeni ambayo iliwaruhusu.

“Hawakupinga na matayarisho yote yalikamilika Jumapili,” alisema.