Habari

Wachina watoa pombe kwa wenye njaa Baringo

April 6th, 2019 2 min read

Na FLORAH KOECH

KIZAAZAA kilishuhudiwa katika kijiji kimoja kinachokumbwa na uhaba wa chakula katika eneo la Tiaty, Kaunti ya Baringo baada ya kampuni moja ya China kuwapa wakazi pombe na chakula.

Kampuni ya Chuanshan international, iliwapa wakazi katoni 20 za pombe iliyotengenezewa China pamoja na magunia 300 ya mahindi na katoni 20 za mafuta ya kupikia.

Wakazi wa kijiji cha Katikit waliokusanyika kugawiwa chakula wakishangilia kwa kupiga makofi na vifijo, mwelekezi wa hafla hiyo alipotangaza kuwa kulikuwa na pia na pombe miongoni mwa chakula cha msaada ambacho kampuni ilitoa.

Mkurugenzi wa kampuni ya Chuanshan, Han Ke alisema, aliamua kujumuisha pombe katika mchango wake wa chakula baada ya kugundua kwamba wakazi wa eneo hilo wanaipenda.

“Wakazi wa eneo hili wanapenda pombe na niliamua iwe sehemu ya chakula cha msaada kwa wanakijiji wanaokumbwa na njaa. Pia tumetoa zaidi ya magunia 300 ya mahindi na mafuta ya kupikia,” alisema Bw Ke.

Kampuni hiyo ilikuwa ikigawa chakula kama sehemu ya jukumu lake la kusaidia jamii ya eneo hilo.

Hata hivyo, kizaazaa kilizuka baada ya wakazi kulewa na kuanza kung’ang’ania magunia ya mahindi ambayo yalinuiwa kugawiwa vijiji saba ambapo wakazi wanakumbwa na uhaba wa chakula.

Miongoni mwa vijiji hivyo ni Katikit, Chemusuk, Chemolingot, Kositei, Seretion, Kapturo na Chemisik.

Baadhi ya wakazi pia waling’ang’ania mikebe ya pombe na kukimbia kuificha vichakani kuepuka wasipokonywe na wenzao.

Wanawake waliokuwa na watoto wachanga ambao walikuwa wakisubiri chakula pembeni waliungana na vijana waliomwaga mahindi wakitaka pombe.

Baadhi ya wanawake na watoto walianza kuzoa mahindi yaliyomwagika kutoka magunia yaliyoraruka baada ya mamia ya wanaume kuvutana kila mmoja akidai chakula hicho kilikuwa cha kijiji chao.

Mkazi ashukuru

Mkazi Bw, Ben Todonyang alishukuru kampuni kwa kuamua kuweka pombe katika mchango wao chakula.

“Tunashukuru sana kupata pombe katika kijiji chetu. Tumekosa chakula kwa muda na pombe hii itatufanya tuchangamke na kusahau shida zetu,” alisema Bw Todonyang.

Mbunge wa Tiaty William Kamket ambaye alihudhuria hafla hiyo alisema chakula cha msaada kilichotolewa na serikali hakikufika eneo hilo kwa sababu ya magari kukosa mafuta.

“Tunashukuru serikali kwa msaada wa chakula lakini magunia zaidi ya 500 bado yako katika maghala ya serikali Chemolingot kwa sababu magari hayana mafuta ya kuyasafirisha. Chakula cha pekee kilichofikia vijiji vinavyokumbwa na njaa ni kile kinachotolewa na wasamaria wema,” alisema.

Hali kama hiyo iliripotiwa kaunti ya Turkana ambapo wakazi wanaendelea kufa njaa licha ya serikali kutoa chakula cha misaada. Viongozi walisema hakuna magari ya kukifikisha kwa wakazi vijijini.