Habari Mseto

Wachoka kuitegema serikali, waungana kujitengenezea barabara

May 30th, 2019 2 min read

Na CHARLES WANYORO

WAKAZI wa kijiji cha Kiebogi, Imenti Kusini, Kaunti ya Meru wameanza kukarabati wenyewe barabara muhimu ya urefu wa kilomita 12 ili kurahisisha uchukuzi katika eneo hilo.

Kwenye mahojiano, walisema tangu barabara hiyo ianze kujengwa miaka 50 iliyopita, haijawahi kufanyiwa ukarabati wowote na hivyo basi kuwasababishia changamoto tele za kiuchukuzi.

Wanakijiji hao wapatao 200 wakijumuisha vijana kwa wazee, wameanza kutengeneza barabara hiyo kutoka soko la Miruriiri kwenye barabara ya Meru kwenda Nairobi katika shughuli wanayotarajia itachukua siku tano.

Wakitumia majembe na koleo, wakazi hao walisema walikuwa wakitatizika kutokana na hali mbaya ya barabara hiyo iliyotengwa kwa mara ya kwanza 1969.

Bi Jennifer Joseph, 65, ambaye ni mmoja wa wanaochimba barabara hiyo alisema waliamua kuchukua hatua baada ya mwanamke aliyekuwa mjamzito kujifungua akiwa barabara hiyo kabla ya kufikishwa hospitalini.

Wiki moja kabla ya tukio hilo, wakazi walilazimika kubeba jeneza lililokuwa na mwili wa mmoja wao baada ya gari kushindwa kupitia barabara hiyo.

Mkazi huyo alisema kwamba huwa wanakarabati barabara hiyo kila mwaka shughuli ambayo imeanza kuwa ngumu kwa sababu ya mashimo makubwa yaliyochukua miaka mingi.

“Kila wakati kukinyesha, maji kutoka juu ya milima hufurika kwenye barabara hii na kuifanya isipitike. Huwa tunalazimika kutembea mwendo mrefu kwa sababu magari hayawezi kufika eneo hili,” alisema nyanya huyo.

Alisema msimu wa mvua, wanafunzi huwa wanasindikizwa kwenda na kutoka shule ili wasianguke kwenye mashimo.

Barabara hiyo inaunganisha vijiji vya Kiune na Kiebogi na soko la Miruriri. Kiune ndiko kuna zahanati muhimu ya wakazi, shule za msingi na sekondari. Bi Carol Kainyu, mkazi anayefanya biashara ya kuuza ndizi alisema wakulima wengi hupata hasara kwa sababu mazao yao mengi hayafiki masokoni.

Wakati huu wakazi waliamua kuchanga pesa kununua chakula cha kupikia wanaochimba barabara hiyo.

Baadhi ya wanawake wamepiga kambi katika boma moja wanakopikia wafanyakazi chai, uji na wali.

“Barabara hii haijawahi kurekebishwa tangu ilipojengwa. Ni matumaini yetu kwamba diwani John Kireria atasaidia kuitengeneza,” alisema Bw Festus Mbae.

Bw Patrick Muthomi, 63, alisema wakazi wanahisi wamebaguliwa kwa sababu wanalipa kodi ilhali hawapati huduma za kutosha.

“Niliwaona wazazi wangu wakichimba barabara hii kwa mikono yao. Barabara katika maeneo mengine zimetengenezwa lakini hakuna kinachotendeka hapa. Hakuna gari linaloweza kupitia barabara hii kunaponyesha, tunateseka na tunaachia Mungu” alisema.