Wachomea Rais picha

Wachomea Rais picha

Ruto apenya nyumbani kwa Uhuru, Raila aendeleza ushawishi Nyanza

VIONGOZI walioongoza kampeni za chama cha tawala cha Jubilee kwenye chaguzi ndogo za maeneobunge ya Bonchari, Juja na wadi ya Rurii wamemuaibisha Rais Uhuru Kenyatta kwa matokeo duni.

Licha ya kujipiga kifua na kutumia polisi kunyanyasa wagombeaji wa vyama vya upinzani, chama hicho hakikushinda hata kiti kimoja kwenye chaguzi hizo tatu, kikiwemo cha eneobunge la Juja katika kaunti ya nyumbani kwa Rais Kenyatta ya Kiambu.

Juja watuma ujumbe kwa rais hali si hali

Mivutano katika kambi ya Jubilee kwenye kampeni za eneobunge la Juja, Kaunti ya Kiambu imeibuka kuwa sababu kuu ya chama hicho kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta kushindwa kwenye uchaguzi mdogo wa Jumanne.

Mwaniaji wa Jubilee, Susan Njeri Waititu, ambaye ni mjane wa aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Francis Munyua Waititu, aliangushwa na George Koimburi

Imefichuka kuwa kampeni za Jubilee ziliongozwa na katibu wa wizara mwenye ushawishi mkubwa, ambaye aliwakilishwa kwenye shughuli hizo na kamishna wa Kiambu, Wilson Wanyanga.

Kutokana na kuwa mradi wa serikali, Bi Njeri alikubaliwa kufanya kampeni zake kama kawaida licha ya kanuni za Covid-19, huku wapinzani wake wakizimwa kukusanyika.

Wengine waliohusika pakubwa katika kampeni hizo za Juja ni Gavana James Nyoro, Mwakilishi wa Wanawake Kiambu Gathoni Wamuchomba, Mbunge wa Kiambu Mjini Jude Njomo na Naibu Gavana Joyce Ngugi. Duru zilieleza Taifa Leo kuwa mbinu za kampeni za Jubilee zilianza kusambaratika tangu mwanzo baada ya tofauti kuibuka kuhusu aliyefaa kuziongoza na ugawaji wa pesa.

Pia Jubilee inalaumiwa kwa kulegeza juhudi zake pale chama cha United Democratic Alliance (UDA) kilipojiondoa kwenye uchaguzi huo kwa kudhani kuwa upinzani ulikuwa umepungua.

Wiki iliyopita, Gavana Nyoro alionyesha imani kubwa kuwa Jubilee ingeshinda bila tatizo aliposema: “Haufanyii kampeni kiti ambacho tayari umeshinda. Mashinani ni Jubilee na wapigaji kura wanajua kuwa mgombeaji wa rais ni Susan Njeri.”

Hapo Jumatano, Mwenyekiti wa vuguvugu la Jubilee katika Kaunti ya Kiambu, Elijah Njoroge, ambaye pia alihusika katika kampeni hizo, alitaja kushindwa kwa Jubilee kuwa ujumbe kwa Rais Kenyatta kuwa mambo sio mazuri mashinani.

“Kile tumeshuhudia leo ni kura ya malalamishi dhidi ya Jubilee, na inabidi rais aje mashinani azungumze na wakazi wa Mlima Kenya,” akasema Bw Njoroge.

Taifa Leo pia imepashwa habari kuwa viongozi wa kampeni hizo walipokutana walizungumzia zaidi kuhusu ugawaji wa pesa kuliko kuhusu jinsi ya kushawishi wapigaji kura, hali iliyozua migawanyiko.

“Tangu mwanzo, uteuzi wa watu wa kuongoza kampeni za Jubilee ulikuwa na kasoro. Nyoro hana mbinu za ushawishi mashinani, Wamuchomba sio maarufu tena kama alivyokuwa 2017, naye Njomo hajui kusisimua watu. Pia hakuna vile tungeshinda tukizozana kila mara,” mdokezi aliyekuwa kwenye kampeni hizo alieleza.

Wapinzani wao wa Peoples Empowerment Party (PEP) chake Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria wanaelezwa walichukua fursa hiyo kuingiza watu wao katika kambi ya Jubilee kuikoroga.

Kambi ya Bw Koimburi pia ilitumia uhusiano wa Bw Kuria na Naibu Rais William Ruto katika kampeni zake, jambo linalotajwa lilichangia kupata kura nyingi kutoka kwa wafuasi wa Dkt Ruto.

Barabara, hati za ardhi, uhuni zakosa kushawishi wakazi kupigia chama cha Uhuru Rurii

Mambo hayakuwa tofauti katika wadi ya Rurii, Kaunti ya Nyandarua, wakati Francis Muraya wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu Rais William Ruto, alipomwangusha mwaniaji wa Jubilee, Peter Thinji Kiriga.

Jubilee ilipoteza viti hivyo licha ya kampeni zake kuongozwa na wakareketwa wakuu wakiwemo mawaziri, magavana na wabunge.

Katika wadi ya Rurii, Gavana Amos Kimunya, ambaye alikuwa akiongoza kampeni za Jubilee aliachwa kinywa wazi baada ya mwaniaji wake kushindwa licha ya raslimali na juhudi walizokuwa wameweka wakati wa kampeni.

Katika kampeni hizo za Jubilee, Bw Kimemia alishirikiana mwenzake wa Laikipia Nderitu Muriithi, Waziri wa Maji Sicily Kariuki, Kiongozi wa Wengi Bungeni Amos Kimunya na wabunge Njuguna Kiaraho (Ol Kalou), Kanini Kega (Kieni) na Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini).

Jubilee ilipoteza kiti hicho licha ya mbinu ilizotumia kushawishi wenyeji kama vile kuzindua miradi ya maendeleo na kuweka maramu barabara katika wadi hiyo.

Katika kipindi hicho cha kampeni, serikali pia ilitoa hati za kumiliki ardhi kwa watu ambao wamekuwa wakiishi katika vijiji vilivyobuniwa wakati wa ukoloni vya Bahati, Turkana na Co-site vilivyoko wadi hiyo ya Rurii.

Siku tatu kabla ya uchaguzi huo, Bw Kimemia na Bw Muriithi waligawa chakula na bidhaa zingine kwa wakazi wa vijiji vya Turkana na Bahati.

Mbinu nyingine iliyotumika ni kundi la Jubilee kufanya kampeni zake kwa njia huru, huku mikutano ya wapinzani wao wa UDA ikivurugwa na polisi.

Kwenye mbinu hiyo, mara baada ya polisi kutawanya kundi la UDA, msafara wa Jubilee ukijumuisha madiwani, wafanyikazi wa kaunti na wanasiasa wengine ulikuwa ukifika na kutoa hotuba za kudunisha yaliyokuwa yamesemwa na wapinzani wao.

Kampeni za UDA ziliongozwa na wabunge Faith Gitau (Nyandarua), Rigathi Gachagua (Mathira), Ndindi Nyoro (Kiharu) na Jayne Kihara (Naivasha).

Ushindi wa UDA huenda ukampa motisha Bi Gitau ambaye ametangaza nia ya kuwania ugavana dhidi ya Bw Kimemia.

KIMEMIA

Dkt Simon Kanyingi, ambaye aliwania ugavana 2017 alilaumu makao makuu ya Jubilee kwa chama hicho kushindwa Rurii.

“Jubilee ilikosea kwa kumtuma Kimemia kuja kuwapa wakazi wa Rurii ahadi mpya na hali za awali hazijatimizwa. Kimemia pia aliwatumia wafanyikazi wa kaunti kufanya kampeni badala ya kuwaunganisha wanasiasa waliochaguliwa kufanya kazi hiyo. UDA ilifanikiwa kwa kuwatumia wakazi wenyewe mashinani,” akaongeza Bw Kanyingi.

Aliyekuwa Meya wa Nyahururu, Peter Thiari alisema Jubilee itazimwa na UDA katika Nyandarua iwapo haitafanya juhudi za kujifufua.

Hapo Jumatano, Kiongozi wa ODM Raila Odinga, ambaye ni mshirika wa Rais Kenyatta serikalini, alishtumu mbinu zilizotumiwa na Jubilee katika chaguzi hizo ndogo.

Bw Odinga alisema baadhi ya watumishi wa umma wenye ushawishi ndio wamekuwa wakiwatumia polisi kutatiza wagombeaji wa vyama pinzani hasa ODM na UDA.

Alisema tabia hiyo inarudisha Kenya katika enzi za udikteta na inapasa kukomeshwa.

Polisi, pesa hazikusaidia Opore kupaa Bonchari

Kushindwa kwa mwaniaji wa chama tawala cha Jubilee, Zebedeo Opore katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Bonchari, Kaunti ya Kisii, kumemuacha Waziri wa Usalama Fred Matiang’i amesononeka katika eneo la Gusii.

Dkt Matiang’i amekuwa mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta tangu 2013 alipoteuliwa waziri, na tangu hapo amepokezwa madaraka zaidi kama vile kushirikisha mipango ya serikali na hata kuongoza mikutano ya Baraza la Mawaziri kwa niaba yake.

Uchaguzi mdogo wa Bonchari ulipojiri baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge Oroo Oyioka, kibarua cha kuongoza juhudi za kuhifadhi kiti hicho ndani ya Jubilee kilimwangukia Dkt Matiang’i.

Licha ya Dkt Matiang’i kutohusika moja kwa moja kwenye kampeni za uchaguzi huo mdogo uliofanyika Jumanne, dalili zote zilionyesha kwamba Bw Opore alikuwa akipigiwa debe na serikali kwa njia nyingi lakini akafeli.

Wakati kampeni za wafuasi wa ODM na UDA zilikuwa zikitawanywa na maafisa wa polisi, hakuna hata mkutano mmoja wa Bw Opore uliohujumiwa.

Wiki iliyopita wakati polisi walipovuruga mkutano wa Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Kisii, Janet Ong’era, Bw Opore alikuwa akifanya mkutano wake uliohudhuriwa na mamia ya vijana katika mkahawa mmoja mjini Kisii bila usumbufu wowote.

Upande wa Jubilee pia uliwatumia machifu na maafisa wa Nyumba Kumi, ambao duru zilieleza walikuwa wamepewa maagizo kutoka kwa wakuu wao wamtafutie Bw Opore kura mashinani.

“Nyinyi mnajua chama cha serikali ni kipi na mnafaa kukiunga mkono kwenye uchaguzi mdogo ujao,” akasema Naibu Chifu wa kata ndogo ya Bogitaa, Bw Zebedeo Ntabo katika hafla moja ya mazishi eneo la Riana.

Naye gavana wa Kisii, James Ongwae alivamiwa nyumbani kwake Alhamisi iliyopita na maafisa zaidi ya 50 wa polisi katika makazi yake ya Maili Mbili.

Gavana Ongwae alikuwa amewaalika nyumbani kwake Seneta wa Kisii Profesa Sam Ongeri, Bi Ong’era na mwenzake kutoka Migori Dkt Pamela Odhiambo.

Utoaji wa bidhaa pia ulishuhudiwa ambapo mnamo Jumamosi iliyopita, baadhi ya watu waliokuwa kwenye msafara mrefu wa Bw Opore waliwapa akina mama bidhaa za nyumbani.

Siku ya upigaji kura, maajenti kadhaa wa ODM na UDA walikamatwa na polisi.

Licha ya kutumia mbinu hizo, Jubilee ilikosa kiti hicho.

ilichotafuta kwa bidii na Pavel Oimeke Obwoto wa ODM akaibuka mshindi.

Mkurugenzi huyo wa zamani wa Halmashauri ya Kudhibiti Kawi na Mafuta (EPRA) alizoa kura 8,049 ilhali Bw Opore alichukua nafasi ya pili na kura 7,279.

Mjane wa Oroo Oyioka, Bi Teresa Bitutu aliridhika na nafasi ya tatu kwa kura 6,964.

Ripoti za Simon Ciuri, Steve Njuguna na Wycliffe Nyaberi

You can share this post!

Arsenal wacharaza Crystal Palace ugenini na kupaa hadi...

Aston Villa wadidimiza matumaini ya Spurs kuwa miongoni mwa...