Wachukuzi walia SGR ikiwanyima biashara

Wachukuzi walia SGR ikiwanyima biashara

NA ANTHONY KITIMO

WASAFIRISHAJI mizigo kwa malori kutoka kwa bandari ya Mombasa wamepata pigo, baada ya serikali kusema mizigo yote inayoelekea Sudan Kusini itaendelea kusafirishwa kwa reli ya SGR pekee.

Hivi majuzi, wenye malori walikuwa wamelalamika kuwa, licha ya amri ya Rais William Ruto kwamba waagizaji mizigo wapewe uhuru wa kujiamulia mbinu ya uchukuzi kutoka bandarini, bado walikuwa wanalazimishwa kutumia SGR.

Sudan Kusini huwa ni ya pili baada ya Uganda kwa utumizi wa bandari ya Mombasa.Kwenye ilani iliyotolewa na Wizara ya Uchukuzi kwa wadau wanaotumia bandari, serikali ilisema makubaliano yaliyowekwa kati ya Kenya na Sudan Kusini kuhusu jinsi mizigo inayoelekea nchi hiyo, itasimamiwa, bado yanazingatiwa.

Kulingana na ilani hiyo ya waziri James Macharia, makubaliano hayo, hayajabatilishwa licha ya agizo lililotolewa na rais wakati alipoapishwa kuhusu usimamizi wa mizigo katika bandari ya Mombasa.

Bw Macharia alieleza kujitolea kwa Kenya kusaidia serikali ya Sudan Kusini kibiashara na kwa uchukuzi wa mizigo na watu kupitia Kenya kuelekea nchi hiyo.

“Serikali ya Sudan Kusini ilitambua Kituo cha Mizigo cha Nairobi kupitia kwa barua ya Februari 25, 2022, iliyotoka kwa Waziri wa Uchukuzi, Madut Biar Yel, ambayo iliwasilishwa kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni nchini mnamo Machi 7, 2022. Kwa hivyo, hii inachukuliwa kuwa maelewano kati ya serikali moja na nyingine,” akasema Bw Macharia, katika ilani iliyoandikwa Oktoba 4.

Kulingana na waziri huyo anayeondoka, Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA), imebainisha kwamba Serikali ya Sudan Kusini haijabatilisha makubaliano hayo.

“Hata maafisa wa ukusanyaji ushuru wa Sudan Kusini bado wako katika Kituo cha Mizigo cha Nairobi kwa hivyo hii inathibitisha kuwa, uchukuzi wa mizigo inayoelekea Sudan Kusini bado ni chini ya makubaliano kati ya serikali moja na nyingine hadi wakati tutakapoambiwa vinginevyo na serikali ya Sudan Kusini,” akaeleza.

Wachukuzi wa mizigo kutoka bandarini walitaka makubaliano hayo yafutiliwe mbali, huku wakimkashifu Bw Macharia na kusema hakuzingatia barua iliyotoka kwa ubalozi wa Sudan Kusini kwa serikali ya Kenya mnamo Juni 15, 2022, wanayodai ilifutilia mbali maelewano hayo.

Sehemu ya barua hiyo ilikuwa imesema mizigo inayoelekea katika nchi hiyo isiwe ikipelekwa katika kituo cha Nairobi bali iendelee kuchukuliwa Mombasa hadi mashauriano zaidi yatakapofanywa.

Madalali wa utoaji mizigo bandarini wamelalamikia msimamo huo wa serikali , na kusema utawanyima biashara Mombasa.

“Agizo hilo litasababisha hasara kibiashara na huenda tukalazimika kuhamia Nairobi,” akasema mwenyekiti wa Chama cha Uchukuzi na Uhifadhi wa Mizigo Kimataifa, Bw Roy Mwanthi.

Mizigo ya Sudan Kusini huchukuliwa kuwa ya thamani kubwa kibiashara kati ya wachukuzi wa mizigo katika bandari ya Mombasa kwa sababu ya wingi wake.

Katika miaka iliyopita, kampuni tofauti zimekuwa zikipokea zabuni ya kusimamia mizigo ya nchi hiyo ikiwemo Compact CFS, Regional Logistics, Siginon Container Freight, Awanad CFS, Mitchell Cotts, Consol Base CFS, Asgher Moulu & Fernando Marquis na Makupa CFS.

Malalamishi kuhusu usimamizi mbaya wa mizigo inayoelekea Sudan Kusini ndiyo yamekuwa zinazosimamia mizigo hiyo mara kwa mara.

  • Tags

You can share this post!

Njaa yalemea raia msaada wa serikali ukichelewa kufika

Wenye vipande vya ardhi Diani waonywa kupoteza endapo...

T L