Habari Mseto

Wachungaji bado wako katika njia panda kuruhusu waumini wasiozidi 100 kanisani

July 13th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WACHUNGAJI wa madhehebu tofauti walikongamana katika shule ya msingi ya Mugumuini Thika, ili kutathmini jinsi ya kurejelea maombi ya pamoja kwa waumini wao.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina.

Bw Wainaina alisema janga la corona limesababisha Wakenya wengi kuwa katika msongo wa mawazo.

“Tunajua hali ya Covid-19 imevuruga kila mtu popote pale na wengi wanastahili kupewa ushauri nasaha. Wachungaji wanastahili kuwa mstari wa mbele kutekeleza wajibu huo,” alisema Bw Wainaina.

Alitoa mwito kwa kila mmoja popote alipo kuzingatia sheria zilizowekwa na Wizara ya Afya ili kukabiliana na Covid-19.

Aliwataka Wakenya wasichukulie jambo hilo kwa mzaha “kwa sababu homa ya corona ipo.”

“Mimi nina rafiki yangu wa karibu ambaye aliangushwa na homa hiyo hatari. Kwa hivyo, kila mmoja awe chonjo kukabiliana na corona,” alisema Bw Wainaina.

Naibu Kamishna wa Thika Magharibi Bw Douglas Mutahi, aliwashauri wananchi watubu dhambi zao.

“Tunastahili tumrudie Mungu wetu kwa unyenyekevu na kuomba msamaha,” alisema Bw Mutai.

Aliwashauri wachungaji kuwa mstari wa mbele kuzungumzia mambo maovu ili Wakristo waweze kuelewa.

” Ninawaomba nyingi wachungaji muwe mstari wa mbele kukosoa maovu na kuhubiri haki na ukweli,” alisema Bw Mutai.

Bw Simon Githioro Njuguna, wa kanisa la PCEA ya Makongeni, Thika alisema kuna changamoto ya kupanga waumini wao kwani kanisa lao lina waumini zaidi ya 2,000 ambao kwa hali ya kawaida huhudhuria ibada ifikapo Jumapili.

“Tutaweka kikao maalum ili kuwa na mbinu mwafaka kuona ya kwamba tunafuata maagizo ya serikali ya kuruhusu waumini wasiozidi 100 kwa wakati mmoja,” alisema Bw Njuguna.

Alisema wakati huu wa kupambana na Covid -19 kuna mengi yanayoendelea katika jamii.

“Kuna mimba za mapema miongoni mwa wasichana wa shule, wazazi popote walipo wamelemewa na mizigo na hata sisi kama wachungaji tunatarajia kutoa ushauri mwafaka kwa wazazi wote walio na matatizo,” alisema mchungaji huyo.

Bw Francis Kilango wa kanisa la Springs of life Church Ministries, Kabati, Murang’a, anatoa mwito kwa serikali kufanya juhudi kutoa vifaa vya kupima halijoto ili wachungaji waweze kuendesha shughuli zao bila shida.

Aliwashauri wazazi wawachunge wana wao popote walipo kwa sababu kwa wakati huu tuko katika wakati mgumu.

Alipendekeza watu waliofikisha miaka 58 na zaidi wapewe pia nafasi wamuabudu Mungu na washirika wengine.

“Mimi naelewa vijana wengi siku hizi hawapendi kuhudhuria kanisa, na kwa hivyo wazee ndio wamejitolea kumwabudu Mungu,” alisema mchungaji Kilango.

Alitoa mwito kwa wazazi wawe macho kwa kuwachunga wana wao hasa wakati huu wanafunzi bado wako nyumbani.

“Tuko katika wakati mgumu wa kimaisha na jambo litakalo tuokoa ni kumwamini tu Mwenyezi Mungu. Kwa wakati huu kila mmoja yuko katika hali ngumu kwa njia moja au nyingine,” alisema mchungaji Kilango.