Wachungaji Thika wawatolea wito Wakenya waiunge mkono serikali

Wachungaji Thika wawatolea wito Wakenya waiunge mkono serikali

NA LAWRENCE ONGARO

WACHUNGAJI kutoka kaunti ndogo ya Thika, wametaka Wakenya kuiombea nchi hii ili serikali mpya iweze kufanikiwa katika kutekeleza ahadi ilizotoa.

Wakiongozwa na Askofu wa Kanisa la Calvary Chosen Centre, Thika, David Gakuyo, walisema serikali mpya ya Rais William Ruto, inastahili kupewa muda wake ili iweze kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.

Alisema “huu sasa ni wakati wa kufanya kazi na kusahau yaliyopita ili tuendelee mbele kama Wakenya”.

“Mimi nilifuata mrengo wa Azimio, lakini baada ya mambo kwenda jinsi yalivyoenda, ninaunga mkono serikali ya Kenya Kwanza kwa sababu ndiyo iliyoko uongozini,” alijitetea Askofu Gakuyo.

Alisema baada ya Rais Ruto kutwaa uongozi, ameleta mabadiliko mengi hasa kwa kuwateua majaji, na kuwakomboa watu wengi waliokuwa hawana usemi kwenye uongozi uliopita.

Alisema sasa amerejea katika kazi ya kuhubiri kwa kishindo akiwashauri waumini wake wamweke Mungu mbele ili “nchi yetu iweze kuinuka ipasavyo”.

Katika hafla hiyo waumini zaidi ya 500 walikongamana katika kanisa la Calvary Chosen Centre ili kusikiliza neno la Mungu.

“Sisi kama Wakenya tuungane pamoja kuona ya kwamba tunaendelea mbele. Chuki za hapo awali zinastahili kusahaulika haraka iwezekanavyo,” alieleza Askofu huyo.

Kuhusu mahindi ya GMO, alisema ni vyema serikali kufanya uchunguzi kupitia wataalam ili chakula kifaacho kiletwe.

“Sisi kama wachungaji tunastahili kuiombea nchi ili tupate chakula bora. Kwa hivyo Rais Ruto anastahili kusitisha mpango huo wa kuingiza mahindi yasiyo halali nchini,” alisema mchungaji huyo.

Askofu huyo aliandamana na wachungaji wengine kama Pasta John Njoroge na Pasta Patricia Wairimu, ambao pia walihimiza waumuni kuwa kitu kimoja.

  • Tags

You can share this post!

Afueni Mombasa kaunti ikirudishia vijana Kazi Mtaani

Mafunzo ya marefarii wa Ligi ya Taifa Divisheni ya Kwanza...

T L