Wachungaji waomba amani idumu Kenya inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu

Wachungaji waomba amani idumu Kenya inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu

Na LAWRENCE ONGARO

WACHUNGAJI wa makanisa wameitaka serikali iwe makini kuhakikisha amani na usalama unadumu nchini.

Wakiongozwa na Askofu wa Kanisa la Glory Outreach Assembly (GOA) la Kahawa Sukari Bw James Kamata, walisema uvamizi unaoendelea eneo la Laikipia Magharibi unatia hofu kwa wakazi wa huko na ni vyema vitengo vya usalama kuingilia kati.

Katibu wa Shirika la muungano wa wachungaji linalofahamika kama Federation of Evangelical and Indigenous Christian Churches of Kenya (FEICCK) Askofu David Munyiri Thagana, aliiomba serikali kuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba uvamizi unaoendelea Laikipia unazimwa haraka iwezekanavyo.

Alisema inasikitisha kuona viongozi fulani wakieneza chuki badala ya kuleta wananchi pamoja.

“Ninatoa wito kwa vijana wawe chonjo wasije wakapotoshwa na viongozi wa kisiasa na badala yake wawe na uzalendo,” alisema Askofu Thagana.

Kwa muda wa mwezi mmoja sasa, wakazi wa Laikipia wamekuwa wakiishi kwa hofu bila kujua la kufanya kutokana na mashambulio yanayofanywa na wavamizi wa kuiba mifugo.

“Sisi kama wachungaji tunaiomba serikali ichukue hatua ya dharura kuona ya kwamba wavamizi hao wanakabiliwa vilivyo na kulinda maisha ya wananchi. Hata wakazi kadha wameuawa na mifugo zao kuibwa katika maeneo hayo,” alifafanua Askofu Kamata.

Wachungaji hao walitoa ushauri kwa wanasiasa kuwa makini ili wasichochee uhasama miongoni mwa wakazi wa Laikipia.

Waliyasema hayo katika kanisa la Glory Outreach Assembly lililoko eneo la Kahawa Sukari.

Askofu Kamata aliiomba Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba viongozi wa Kisiasa wanahubiri amani.

“Wakati huu tunapoelekea uchaguzi mkuu tunastahili kuwa pamoja kama wananchi. Kila mmoja wetu anahitaji mwenzake,” alisema Askofu Kamata.

Naye Askofu Samuel Njiriri, alisema FEICCK itafanya hamasisho kwa wapigakura ili wawe na mwelekeo mwafaka wakati wa kupiga kura utakapofika.

“Tunapongeza juhudi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa hatua iliochukua ya kutaka kuandikishaji vijana wapatao 6 milioni ili wajiandae kwa upigaji kura ifikapo mwaka ujao wa 2022.

“Sisi kama wachungaji tutafanya juhudi kuona ya kwamba vijana wanapewa hamasisho ili ifikapo wakati huo wafanye maamuzi yafaayo,” alisema Askofu Njiriri.

Alisema wachungaji wataendelea kuiombea nchi ya Kenya ili iweze kufanya uchaguzi wa amani bila vurugu.

“Tutaedelea kuwarai vijana kote nchini kuwa makini ili wasikubali kutumiwa vibaya na viongozi, lakini badala yake wafanye uamuzi ufaao,” alifafanua Askofu Njiriri.

Maaskofu hao pia walitoa wito kwa viongozi popote walipo kuendesha kampeni za amani bila matusi.

You can share this post!

Juventus yaadhibu AS Roma ya kocha Jose Mourinho kwenye...

WARUI: Tuzo ya Nobel ya Abdulrazak ushindi kwa elimu Afrika

T L