Habari

Wachunguzi wa kifo cha Tecra Muigai wapewa siku 30 zaidi

June 10th, 2020 1 min read

Na KALUME KAZUNGU

WACHUNGUZI wa kesi inayomkabili Omar Lali, mpenzi wa binti ya wamiliki wa kampuni ya Keroche Breweries, marehemu Bi Tecra Muigai, wamepewa siku 30 zaidi za kuendeleza na kukamilisha uchunguzi wao.

Uamuzi huo uliafikiwa baina ya mawakili wa Lali wakiongozwa na Bw Yusuf Aboubakar na ofisi ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na ile ya Uchunguzi wa kesi za Uhalifu (DCI).

Wakati wa kikao cha korti kilichotekelezwa Jumatano kupitia video na kuongozwa na Hakimu wa Mahakama ya Lamu, Allan Temba, pande zote zimeafikiana kutoa muda wa mwezi mmoja kwa wachunguzi na DPP kukamilisha uchunguzi wao kuhusiana na iwapo Lali alihusika kwa njia yoyote na ajali iliyosababisha kifo cha Bi Tecra kilichotokea Mei 2, 2020.

Hata hivyo, Lali ataendelea kuwa huru katika kipindi chote cha mwezi mmoja wa uchunguzi.

Siku moja baadaye baada ya kifo cha mwanadada huyo, Lali alikamatwa na amekuwa akizuiliwa na polisi kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja kabla ya kuachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 mnamo Mei 27.

Ukuruba wa Bi Tecra na Lali – ambaye kazi yake ni kutoa huduma za watalii wanaozuru ufuo wa bahari eneo la Lamu – ulianza katikati ya mwaka 2019.

Wawili hao walikuwa wakionekana kwenye maeneo ya burudani wakijivinjari kwa vinywaji kabla ya Bi Tecra kukumbwa na mkasa wa ajali hiyo ya kuanguka kutoka kwa ngazi za nyumba moja ya kibinafsi walimokuwa wakiishi na Lali.

Baadaye aliwahishwa hospitalini Nairobi lakini akafariki kutokana na majeraha mabaya ya kichwa aliyopata baada ya kuanguka eneo hilo la Shella.

Bi Tecra alizikwa katika hafla iliyoandaliwa nyumbani kwao huko Naivasha mnamo Mei 16, 2020.