Makala

Wachuuzi matapeli wanaouza samaki waliooza barabarani   

February 26th, 2024 2 min read

NA RICHARD MAOSI

WASAFIRI wameomba serikali kupiga msasa wauzaji wa samaki, ikifichuka kuwa baadhi ya matapeli wanatumia fursa hiyo kuwauzia wateja samaki ambao wameoza.

Ndiposa unatakiwa kuwa makini unaponunua kitoweo cha samaki katika maeneo wazi, hasa kwenye barabara ya Nairobi-Nakuru.

Bw Aldrine Kemboi mkazi wa Kinungi ambaye pia ni dereva kati ya Naivasha na Limuru na anaunga mkono suala la wauzaji kutengewa sehemu maalum ya kufanyia biashara zao.

“Badala ya kuendesha shughuli zao katika eneo wazi, serikali iweke mikakati ya kutengeneza soko la kuuza samaki, ili kuwadhibiti matapeli,” akasema akaambia Taifa Leo Dijitali kupitia mahojiano ya kipekee.

Maeneo maalum ya kuuza samaki yatawafanya wachuuzi kuwajibika na pia kudumisha usafi wa hali ya juu, ikizingatiwa kuwa baadhi ya maeneo ya kufanyia biashara yenyewe ni karibu na sehemu za kutupa taka.

“Hapa tunaona kama baadhi ya wachuuzi wanachezea afya zetu kwa sababu wametangamana na matapeli ambao huwauzia wateja samaki wanaotoa uvundo,” Bw Kemboi akateta.

Anasema uuzaji wa samaki kiholela barabarani unafaa kudhibitiwa kwani unaweza kusababisha mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu.

Isitoshe, barabarani sio mazingira faafu kwani angani kumezagaa vumbi nyingi na moshi unaotokana na mafuta ya dizeli au petroli.

Bi Alice Mbote mkaazi wa Embu kwa upande mwingine anasema aliacha kununua samaki wa kuchuuzwa barabarani siku moja alipouziwa samaki ambaye ameoza katika sehemu moja.

Alipofika nyumbani alishindwa kuvumilia uvundo mkali, hivyo basi ikamlazimu atupe kitoweo ambacho alikuwa amenunua Sh350 karibu na mto Sagana.

Alisema kisa hicho kilikuwa mara yake ya tatu kupitia changamoto kama hiyo.

Kuanzia siku hiyo amejifunza namna ya kukagua samaki sokoni kabla ya kununua.

Miaka mitano iliyopita, Maafisa wa Afya ya Umma walipiga marufuku uuzaji wa samaki katika eneo la Kinungi barabara ya Nairobi-Nakuru

Hata hivyo, vijana wengi walipinga hatua hiyo wakidai sekta ya uvuvi ilikuwa ikitengeneza nafasi nyingi za ajira.

Aidha, wanaendeleza biashara hiyo licha ya onyo la serikali.