Habari Mseto

Wachuuzi Nairobi waandamana kupinga kuhangaishwa na askari wa kaunti

March 14th, 2018 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

WACHUUZI walemavu Jumatano waliandamana jijini Nairobi kupinga hatua ya askari wa jiji kuwahangaisha.

Wachuuzi hao ambao wengi wao wanauza premende na kushona viatu walishutumu Gavana Mike Sonko kwa kuruhusu maakari wao kuwapokonya bidhaa zao.

Wachuuzi hao waliokuwa wamejawa na hamaki walishangaa kwa nini serikali ya kaunti inawahangaisha ilhali ombaomba wakiachwa kuendelea kuomba fedha kwa wapiti njia.

“Sisi hatutaki kuomba, tunauza bidhaa zetu ili kupata fedha za kulisha watoto wetu. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba, tunahangaishwa na omba omba ambao wengi wao wanatoka nchi jirani ya Tanzania wakiachwa kuendelea kuhangaisha wapiti njia,’ akasema Susan Busaka ambaye ni muuzaji wa peremende.

Bi Busaka alisema hujipatia Sh300 kwa siku kutokana na biashara hiyo.

John Njenga Ndung’u ambaye anang’arisha viatu katika mtaa wa Tom Mboya alisema maaskari wa kaunti walipokonya vifaa vyake vya kazi na kumwacha na kumfanya kukosa jinsi ya kujikimu kimaisha.

“Walikuja maaskari watano wakabeba vifaa vyangu vya kazi. Sasa hawa maaskari wanadhani mimi nitakula nini pamoja na watoto wangu,’ akasema Bw Ndung’u aliyejawa na hamaki.

Naye George Mwangangi alilalama kuwa maaskari hao walimpokonya mifuko yake ya thamani ya Sh1,000 aliyokuwa akiuza karibu na Jumba la Afya centre.

“Walinipokonya mifuko yangu hivyo nilipata hasara ya Sh1,000,” akasema.

Baada ya kupiga kelele nje ya afisi za serikali ya kaunti, Afisa Mkuu wa Wafanyakazi wa Kaunti Kamau Mugo alijitokeza na kusikiza malalamishi yao.

Bw Mugo aliahidi kuanzisha uchunguzi kuhusiana na madai ya kuwanyanyasa walemavu jijini.