Wachuuzi wa ahadi hewa

Wachuuzi wa ahadi hewa

Na WAANDISHI WETU

WANASIASA nchini sasa wameanza kutoa ahadi za kila aina kwa wananchi ili kuwanasa kwenye ndoano zao huku uchaguzi mkuu wa urais wa 2022 unapozidi kukaribia.

Mtindo huo umeanza kudhihirika hasa miongoni mwa wanasiasa maarufu ambao wametangaza nia za kuwania nyadhifa kubwa kama urais na ugavana.

Baadhi ya vigogo ambao wametangaza kuonyesha azma ya kuwania urais ni Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi (Amani National Congress).

Baadhi ya magavana pia wametangaza nia ya kuwania urais, miongoni mwao wakiwa Hassan Joho (Mombasa), Dkt Alfred Mutua (Machakos), Wycliffe Oparanya (Kakamega), Mwangi wa Iria (Murang’a), Kivutha Kibwana (Makueni) na wengineo.

Wadadisi wanasema ahadi zinazozidi kutolewa kiholela na wanasiasa ni njia za wanasiasa hao kuwapumbaza Wakenya ili kunasa kura zao.“Hizi ni hadaa za kawaida ambazo wanasiasa hao wamezoea kuwaeleza Wakenya. Hawana lolote jipya hata kidogo,” anasema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Mwanauchumi Tony Wetima anasema baadhi ya ahadi hizo haziwezi kutimilika kamwe.Akitoa mfano wa ahadi kubwa za kifedha kwa vijana na wanawake, Bw Wetima alisema hakuna kiongozi anayeeleza kuhusu mbinu atakazotumia kupunguza deni la taifa na kuwarahisishia maisha Wakenya.

“Lazima wanasiasa hao wawaeleze Wakenya kuhusu upunguzaji wa deni la taifa, kwani hilo ndilo suala kuu linaloathiri ukuaji wa uchumi,” akasema.

Kwenye kampeni zake, Dkt Ruto amekuwa akiwaahidi Wakenya kuimarisha uchumi kwa njia itakayompa mwananchi wa kawaida kipaumbele.

Dkt Ruto pia ameahidi kutenga Sh200 milioni kwa kila eneobunge ikiwa atashinda urais. Ikiwa maeneobunge yatabaki 290 kama yalivyo kwa sasa, Dkt Ruto anasema kuwa kila mwaka atakuwa akitenga Sh58 bilioni, na iwapo maeneo hayo yataongezwa hadi 390 kama inavyopendekezwa na BBI, kiasi hicho kitapanda hadi Sh78 bilioni.

Hata hivyo, wakosoaji wake wanashangaa kwa nini anatoa ahadi za aina hiyo sasa ilhali amekuwa serikalini tangu 2013 ambapo utawala wake na Rais Uhuru Kenyatta uliahidi vijana mamilioni ya nafasi za ajira ila hawajazitimiza hata kwa kiwango kidogo.

Licha ya kuwa mkosoaji mkubwa wa Naibu rais, Bw Odinga pia amejipata lawamani kwa kauli yake kuwa yeye hayuko serikalini, kwa hivyo asisukumiwe mzigo wa makosa yaliyotendeka serikalini tangu 2017, akiahidi makuu wakati marekebisho ya katiba yatakapofanywa.

Hii ni licha ya baadhi ya wandani wake wa karibu kupata teuzi muhimu serikalini ikiwemo ndani ya bunge la seneti na la taifa.Wabunge wa ODM walikuwa miongoni mwa wale waliofaidika kutokana na mageuzi yaliyofanyiwa uongozi na uanachama wa kamati za Bunge la Kitaifa mwaka uliopita.

Hili ni baada ya wabunge wanaomuunga mkono Dkt Ruto kutolewa kwenye kamati hizo.Kimsingi, nafasi hizi zingewawezesha wandani hao wa Bw Odinga kutoa mchango mkubwa kuhusu sera bora za uongozi.

Kwenye mageuzi ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais Kenyatta Jumatano, Mabw David Osiany na Eric Wafukho waliteuliwa kama manaibu waziri katika wizara za Biashara na Fedha mtawalia. Wawili hao ni miongoni mwa washirika wa karibu wa Bw Odinga ambao wamevuna nyadhifa serikalini tangu alipoweka maelewano na Rais Kenyatta, almaarufu handisheki.

Bw Musyoka naye amekuwa akiwaahidi Wakenya atawaruhusu kuendesha shughuli za kibiashara kwa saa 24.V ilevile, amekuwa akiahidi kuimarisha umoja na uthabiti wa kisiasa nchini kutokana na tajriba yake pana kama mpatanishi katika nchi zilizokumbwa na mizozo kama Sudan Kusini.

Hata hivyo, anakosolewa kwa kutochangia hayo alipohudumu kama makamu wa rais kati ya 2008-2013 katika serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki.Kwa upande wake, Bw Mudavadi amekuwa akijinadi kama “mwanasiasa mwadilifu” atakayetumia ujuzi wake mwingi kwenye siasa kuimarisha uchumi.

Licha ya hilo, jina lake limetajwa kwenye sakata kadhaa za ufisadi, miongoni mwao zikiwa za uuzaji tata wa ardhi ya makaburi ya Lang’ata, Nairobi mnamo 2010 ambapo serikali ilidaiwa kupoteza Sh283 milioni.

Bw Mudavadi pia amekuwa akilaumiwa kwa kutochukua hatua zifaazo kuzuia ufisadi alipohudumu kama Waziri wa Fedha kati ya 1993 na 1997. Ni wakati huo ambapo sakata ya ufisadi ya Goldenberg ilipofanyika, ambapo Kenya ilipoteza mabilioni ya fedha.

Seneta Gideon Moi (Baringo), ameahidi kufufua mpango wa kuwapa wanafunzi maziwa ya bure, maarufu kama “Maziwa ya Nyayo” endapo atachaguliwa kuwa rais.

Mpango huo unahusishwa na babake, marehemu Daniel Moi.Hata hivyo, mpango huo tayari unaendeshwa na baadhi ya serikali za kaunti kama vile Mombasa na Nyandarua.

Bw Joho ameahidi kutenga Sh300 bilioni kuimarisha mikakati ya kuwainua kiuchumi vijana na wanawake.Wataalamu wa masuala ya uchumi wameonesha tashwishi kuhusu namna atakavyotimiza hili, ikizingatiwa imekuwa kibarua kwa Serikali ya Kitaifa kutoa kiasi kama hicho cha fedha kwa serkali za kaunti.

Dkt Kidero naye amesema atafanya kila awezalo kuchangia maendeleo katika Kaunti ya Homa Bay, akishikilia kuwa “huko ni nyumbani” ikiwa atashinda ugavana kwenye uchaguzi ujao. Alitoa kauli iyo hiyo 2013 alipowania ugavana Nairobi alipowaambia wakazi kuwa yeye ni jogoo wa jiji kuu.

Ripoti za Mwangi Muiruri, Wanderi Kamau na Eric Matara

You can share this post!

Ruto akubaliana na Raila kuwa kaulimbiu ya...

Aliyejifanya Mhindi Facebook ashtakiwa kwa ubakaji