Habari Mseto

Wachuuzi waendelea kukaidi marufuku ya plastiki

September 27th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

MAMLAKA ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (Nema), imewaonya wafanyabiashara jijini Mombasa, ambao wamerejelea biashara ya mifuko ya plastiki, licha ya marufuku ya serikali.

Akizungumza na Taifa Jumapili, Mkurugenzi wa mamlaka hiyo katika Kaunti ya Mombasa, Bw Samuel Lopokoiyit, alisema lengo la marufuku hiyo mwaka 2017 ilikuwa kuyalinda mazingira.

“Tumekuwa tukifanya uvamizi katika masoko na baadhi ya kampuni zinazotengeneza bidhaa hizo, tulifaulu kuwatia watu wachache mbaroni, lakini bado biashara hiyo inaendelezwa,” akasema.

Alitaja wengi wa wanaotumia mifuko hiyo ni wafanyabiashara wadogo wanaohusika nabiashara za vyakula, matunda na mboga.

“Wanawake wanaopika viazi karai wanawatilia wateja wao bidhaa hizo katika mifuko ya plastiki bila kujali athari za kiafya wanazowaeka wateja wao,” akasema.

Kulingana na wataalamu wa afya, chakula cha moto kinapowekwa katika karatasi ya plastiki huchanganyikana na kemikali zilizotumika kutengezea mifuko hiyo na ambazo zinapomezwa, zinaweza kusababisha maradhi ya saratani, kizazi au hata moyo.

Mkurugenzi huyo alisema wameshirikiana na maafisa wa polisi na serikali ya Kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa wanakomesha wanaoshiriki biashara hiyo.

“Soko la Kongowea liko na wafanyabiashara sugu ambao wanatumia mifuko hiyo na hata kuwauzia wenzao. Mwanzoni mwa mwaka tuliwavamia na kupata wachuuzi kadhaa ambao tuliwafikisha mahakamani,” akasema.

Serikali imeweka adhabu ya kifungo cha miaka minne kwa atakayepatikana akishiriki biashara hyo au kutozwa faini ya hadi Sh100,000.