Michezo

Wadadia LG kupigania pointi sita

October 3rd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Wadadia LG Mumias wikendi hii itakuwa mbioni kutafuta pointi sita muhimu itakapocheza mechi mbili kwenye kampeni za kufukuzia ubingwa wa Soka ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL).

Wadadia LG ambayo hutiwa makali na kocha, Richard Sumba Jumamosi hii imeratibiwa kutifua vumbi dhidi ya Kibera Girls Soccer Academy (KGSA) kisha itakutanishwa na Spedag FC Jumapili katika uwanja wa Stima Club Thika Road, Nairobi.

KGSA na Spedag FC kila moja itaingia mjengoni ikijivunia kusajili ufanisi wa goli 1-0 na 2-1 dhidi ya Makolanders FC na Kisumu Allstarlets mtawalia wiki iliyopita.

”Ninaamini warembo wangu watafanya kazi nzuri hasa kuvuna ushindi wa alama zote ili kujiongezea tumaini la kusonga mbele,” kocha huyo wa Wadadia LG alisema na kuongeza lazima wajitahidi kisabuni ili kutimiza azimio hilo.

Wachezaji wa Kayole Starlets ambao wikendi hii watacheza na Spedag FC kwenye mechi ya Soka ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL). Picha/ John Kimwere

Wadadia LG imekamata nafasi ya tisa kwa kuzoa alama 24, moja mbele ya Eldoret Falcons.

Spedag FC ambayo imeketi katika mduara hatari kati ya vikosi zinazoshikilia nafasi tatu za mwisho kabla ya kukabili Wadadia LG, Jumamosi hii imepangwa kushuka dimbani kucheza na Kayole Starlets uwanjani Stima Club.

Kwenye msimamo wa ngarambe hiyo, Gaspo Womens ingali kifua mbele kwa kukusanya alama 64, tatu mbele ya mabingwa watetezi, Vihiga Queens baada ya kucheza mechi 24 na 22 mtawalia.

Trans Nzoia Falcons inafunga tatu bora kwa kusajili pointi 58, moja mbele ya Thika Queens kutokana na mechi 23 na 25 mtawalia.