Habari Mseto

Wadau wa masomo ya juu wakongamana MKU

February 26th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO
CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kinaendeleza mradi wa hamasisho la masomo ya juu linalojikita kwenye maswala ya Afrika kwa jina la Africa Higher Education Leadership in Advancing Inclusive Innovation for Developement (AHEAD).
Mradi huo wa AHEAD ni wa kuhamasisha wasomi kuhusu miradi tofauti ya kimasomo na ulizinduliwa rasmi mwaka wa 2018 na utaendelea hadi mwaka wa 2021.
Kulingana na naibu chansela wa MKU Profesa Stanely Waudo, mpango huo unajumuisha pia vyuo vikuu vya nchi za nje kama Romania, Poland, Uingereza,  na Italia, bila kusahau Bulgaria.
Katika mpangilio huo, kuna vyuo vikuu vitano kutoka nchini Kenya, vyuo viwili kutoka Tanzania, na vitatu kutoka Uganda.
Mradi huo una maono makubwa ya kuzindua maswala mengi ya masomo yanayohusiana na ubunifu na maendeleo katika vyuo hivyo vilivyotajwa kutoka nchi tatu za Afrika Mashariki.
Prof Waudo ambaye aliongoza hafla hiyo MKU, mjini Thika, aliipongeza mradi huo wa AHEAD akisema litawapa mwangaza washika dau wote kuhakikisha ya kwamba wanapata mafunzo thabiti ya ubunifu na utafiti kwa sababu ni ushirikiano wa vyuo  vingi na washika dau wenye ujuzi tele.
“Nina furaha kuona ya kwamba hii ni hatua kubwa iliyochukuliwa ambayo italeta mwongozo mwema wa kielimu kupitia ubunifu na utafiti,” alisema Prof Waudo.
Utumizi
Alisema ujuzi utakaopatikana katika mradi huo utakuwa na umuhimu wake kwani wote watakaopata ujuzi kutoka hapo watauweka mahali pafaapo katika jamii.
Alizidi kueleza kuwa kuna haja ya kuwa na wajuzi wengi katika nyanja ya kiufundi.
Alisema Kenya Association of Manufacturers (KAM) wanafanya ushirikiano na shirika la GIZ kwa minajili ya kuongezea ujuzi kamili kwa wale wanaojifunza masomo ya kiufundi
Dkt Bibianne Waiganjo ambaye ni naibu wa Naibu wa Chansela kwa upande wa elimu alisema bidhaa nyingi zinazonunuliwa kutoka China huwa ni ujuzi wa wanafunzi ambao wanapata katika masomo ya kiufundi mapema.
Umuhimu wa mradi huo kwa jumla ni kuona ya kwamba unaboresha usimamizi bora, uongozi, mafunzo, na utafiti  utakaoboresha utendakazi wa nchi ya Kenya, Tanzania na Uganda kwa wanafunzi watakaofanya utafiti wao wa kina na kutoka na ujuzi kamili wa kutamanika popote ulimwenguni.
Mradi huo unasimamiwa rasmi na mkurugenzi wa AHEAD Dkt Peter Kirira ambaye alitunukiwa mikoba ya kuwa meneja  mkuu wa mpango huo.