Wadau walia sheria za Covid zawafinya

Wadau walia sheria za Covid zawafinya

WINNIE ATIENO na ALEX KALAMA

BAADHI ya wananchi wameilaumu serikali kwa kuendelea kuweka kanuni kali za kuepusha maambukizi ya virusi vya corona, badala ya kuzilegeza ili kufufua uchumi.

Wiki iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuongeza muda wa utekelezaji wa kanuni za kuepusha maambukizi hayo, ikiwemo kafyu inayodumu kuanzia saa nne hadi saa kumi usiku kila siku.

Wadau katika sekta za utalii, burudani na viongozi wa kidini wamesema serikali inafaa kujikakamua kuhakikisha idadi kubwa ipasavyo ya wananchi wanapata chanjo dhidi ya ugonjwa huo badala ya kuendeleza kanuni zinazoathiri uchumi wa nchi.

Wamiliki wa baa, mikahawa na sehemu za kuvinjari wameitaka serikali kuwaruhusu kuhudumu kama kawaida hasa baada ya magari ya uchukuzi ya umma kuruhusiwa kubeba idadi kamili ya abiria.

“Tunataka usawa. Tunamwomba Rais Kenyatta kuturuhusu kuhudumu ili tuokoe biashara zetu,” alisema Katibu wa Muungano wa Wamiliki wa Baa katika Kaunti ya Mombasa, Bw Kennedy Mumbo.

“Wafanyakazi wetu wameachwa bila ajira sababu ya corona, biashara zimefungwa, sekta hii inaumia sana,” akaongeza. Alisema licha ya serikali kuwaruhusu kuhudumu hadi saa tatu usiku ambapo wanatakiwa kufunga biashara zao, polisi huwakamata kabla saa hizo kuisha.

“Polisi wanatuagiza kufunga ifikapo saa moja usiku. Asilimia 60 ya baa zimefungwa Kaunti ya Mombasa sababu ya changamoto za biashara wakati huu wa janga la corona,” alisema.

Baadhi ya viongozi wa kidini walitaka pia maabadi yaruhusiwe kuwa na idadi kamili ya waumini.

Wakiongozwa na Kasisi Pascal Mwakio wa Kanisa Katoliki la St Patrick mjini Kilifi, viongozi hao walisema si haki kwa sekta ya uchukuzi pekee kulegezewa masharti huku nyumba za ibada zikibanwa.

“Hakuna sababu ya kuendelea kuzuia watu kukaa kwa karibu makanisani ilhali sehemu nyingine mambo yamefunguliwa. Kuzuia usambazaji na uenezaji wa virusi unahitaji nidhamu ya mtu binafsi,” alisema Bw Mwakio.

Msimamo huo uliungwa mkono na Katibu wa Baraza la Waislamu nchini (SUPKEM) tawi la Kilifi, Bw Rashid Mohamed. “Sote tunasema wale wamefunguliwa na sisi pia tufunguliwe, tuachwe tufanye mambo yetu,” alieleza Bw Mohammed.

You can share this post!

Lusaka apuuza uvumi anamezea useneta Bungoma

Man-United wakabwa koo na Southampton ligini