Wadau wataka serikali ifufue mpango wa chakula kwa wanafunzi

Wadau wataka serikali ifufue mpango wa chakula kwa wanafunzi

NA MAUREEN ONGALA

WADAU wa elimu katika Kaunti ya Kilifi wameitaka serikali ya kitaifa kufufua mpango wa kuwapa chakula wanafunzi katika shule za msingi kama njia mojawapo ya kutatua changamoto ya watoto kuhudhuria masomo yao kwa sababu ya njaa.

Pia, wameitaka serikali kuimarisha miundo msingi shuleni, ili kuwapa wanafunzi mazingira bora ya kusomea.

Kulingana na wadau hao, hatua hiyo pia itachangia kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule hizo.

Kaunti ya Kilifi ni mojawapo ya kaunti zilizoathirika pakubwa na ukame huku wakazi wakiteseka kwa makali ya njaa na ukosefu wa maji, hali ambayo imechangia ongezeko katika idadi ya wanafunza wanaoacha shule huku wengine wakikosa kwenda shule kabisa.

Akizungumza katika hafla ya kutoa vitabu katika shule ya Mapawa katika wadi ya Junju, eneobunge la Kilifi Kusini mwanamitindo mashuhuri nchini, Bi Ajuma Nasenyana alisema wanafunzi watasoma vizuri wakiwa wameshiba.

Bi Ajuma alitoa ufadhili wa vitabu 3,000 vya kuandikia kupitia wakfu wake wa Ajuma kwa ushirikiano na kampuni ya Chipper Cash Across Border Payment.

“Njaa na ukosefu wa miundomisingi bora huchangia watoto wengi kukosa motisha ya kuendele na masomo yao na wakati mwingine wanafunzi hulazimishwa kuhama kutafuta shule nzuri,” akasema.

Alitoa mfano wa shule hiyo ya Mapawa ambayo haina madarasa ya kutosha a.Alisema kutokuwa na mpango wa kuwapa watoto chakula umeathiri idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule hiyo, hali ambayo imechangiwa na umaskini mkubwa miongoni mwa wakazi katika eneo hilo.Shule hiyo iliyojengwa mwaka 1974 , ina wanafunzi 340 pekee.Licha ya kuwa madarasa yamezeeka, ina vyoo 5 pekee vilivyozeeka na hutumiwa na walimu pamoja na wanafunzi.

Choo kimoja kimebomoka na kuatarisha maisha ya wanafunzi iwapo kitaendelea kutumika.Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bi Philomena Chome alisema kuwa idadi hiyo imekuwa ikipungua kwa sababu ya umaskini.

Bi Chome alisema wanafunzi huenda shuleni matumbo wazi kwa sababu wazazi wao hawana pesa za kununua chakula.

“Hapo kitambo tulipokuwa tunawapa wanafunzi chakula, idadi hii iliongezeka kila siku, lakini tulipoacha wanafunzi wakaanza kukosa kuja shuleni na kuamua kuketi nyumbani kwa sababu ya njaa.

“Tunatoa wito kwa serikali mpango huo urejeshwe na itakuwa msaada mkubwa sana kwa sababu mtoto akikosa chakula nyumbani atakuwa na uhakika kuwa atakula shuleni,” akasema Bi Chome.

Alishukuru mchango huo wavitabu na kusema kuwa ni msaada mkubwa kwa shule hiyo kwani watoto wengine hawana uwezo wa kununua vitabu na mara kwa mara huhangaika wakiwa darasani.

“Shule hii inapatikana katika jamii ambayo ina umasikini mkubwa na wakati mwingine ni changamoto kwa wazazi wao kupata pesa ya kununua kitabu na kalamu.Hali hii ni changamoto kubwa sana na huathiri pakubwa matokeo yako,” akasema.

Mwenyekiti wa bodi ya wazazi Bw Anthony Muli alisema baadhi ya wanafunzi hukosa chakula kwa siku tatu huku wakilazimika kuvumilia makali ya njaa wakiwa shuleni.

“Ikifika saa nne asabuhi utawakuta watoto wanasinzia kwa sababu ya njaa,wengine huanguka na huzimia asubuhi katika mkutano na walimu,”akasema.

Mkurugenzi msimamizi wa Chipper Cash nchini Kenya na Tanzania Bw Leon Kiptum alisema wanatoa msaada wa vitabu kwa takribani wanafunzi 3,200 na vitabu 15,000.

Bw Kiptum alisema kuwa walilenga kupeana vitabu takribani 60,000 kufikia mwisho wa mwaka huu kupitia wakfu wa Ajuga.

Kulingana na Bw Kiptum ni kuwa kampuni hiyo imewekeza takribani Sh7.5 milioni katika wakfu wa Ajuga ili kuwapa watoto kutoka familia maskini katika kaunti zilizotengwa nchini kupata vitabu na kuboresha kiwango cha elimu.

“Kampuni yetu inajali elimu kwa sababu waanzilishi wetu ni waafrika amabao waliendeleza masomo yao huko Marekani , na kwa hivyo elimu ni swala nyeti kwao kwa sababu iliwasaidia kuwa wanabiashara wakubwa,” akasema.

Alieleza kuwa wataendeleza zoezi hilo katika kaunti ya Taita Taveta ,Mombasa,Kilifi na Lamu.

Baada ya ukanda wa Pwani wataelekeza zoezi hilo katika eneo la Magharibi kisha eneo la Kati nchini.

Bw Kiptum alisema kuwa kampuni hiyo iko katika mikakati ya kupata lenseni ya kupanua kazi zake nchini huku ikilenga kuanzisha mpango wa kupeana ufadhili wa elimu kwa wanafunzi kutoka familia maskini.

mongala@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaruhusu uagizaji wa mahindi kutoka nje

TUSIJE TUKASAHAU: Wadau wahusishwe kikamilifu kuangazia...

T L