Wadau wateta kampuni ya Joho kupewa kandarasi

Wadau wateta kampuni ya Joho kupewa kandarasi

ANTHONY KITIMO

KAMPUNI ya kibinafsi inayohusishwa na familia ya Gavana Ali Hassan Joho hatimaye imechukua usukani wa kituo cha mizigo jijini Nairobi kilichojengwa kwa kutumia pesa za umma kupitia mkataba unaozingirwa na utata huku wadau katika sekta hiyo wakilalamikia dhidi ya hatua hiyo.

Shirika hilo mjini Mombasa kwa jina Autoport Freight Terminals Ltd, limeidhinishwa na Kenya Railways Corporation (KRC) kutumia kivyake Nairobi Freight Terminals (NFT), iliyo karibu na kituo cha Standard Gauge Railway (SGR) Syokimau, na kuwafungia wahusika wengine wanaotumia huduma za usafirishaji mizigo kupitia reli hiyo mpya.

Kupitia notisi kwa Mamlaka inayosimamia Bandari Nchini (KPA) iliyoandikwa tarehe 17 Agosti 2021 ikiomba kuteuliwa kusafirisha mizigo kupitia kituo cha NFT katika kituo cha M/S Autoports Freight, kampuni hiyo iliyopunguziwa ada 2018, itaanza kushughulikia mizigo yote ya kontena na ya kawaida kuanzia Oktoba mwaka huu.

“KPA imepokea ombi kutoka kwa KRC kuhusu kukupa mawasiliano rasmi ya kuruhusu wasafirishaji wa mizigo/au wanaoagizia mizigo kutoka kwa kituo cha upakiaji kuelekea KR Nairobi Freight Terminal (NFT). Kituo hicho kitaendeshwa na M/S Autoports Freight Terminal (AFT) na kimeunganishwa na reli ya SGR. Hatua hii itaruhusu waagizaji zaidi wa bidhaa kutumia SGR,” kilisema kijisehemu cha notisi kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa KPA, John Mwangemi, iliyotumiwa Mkurugenzi wa Kenya Shipping Agent Association, Juma Tellah.

Kulingana na notisi hiyo, waagizaji bidhaa watahitajika kuidhinisha Mswada wa Upakuaji Mizigo katika NFT Autoports Freight Terminal-Nairobi ili mizigo yao isafirishwe kuenda Nairobi na kampuni hiyo inayohusishwa na Bw Joho.

Kupitia notisi rasmi, Bw Mwangemi alisema NFT ina uwezo wa kushughulikia mizigo ya kontena na ile ya kawaida, ina bohari na kituo cha kisasa cha kushughulikia kontena, na vilevile kituo hicho kitasheheni mashirika ya serikali yanayohusika na mizigo kama vile Mamlaka ya Kukusanya Ushuru Nchini (KRA) na Shirika linaloshughulikia Ubora wa Bidhaa (KBS).

Alisema NFT inatarajiwa kuanza kazi Oktoba 2021 hatua ambayo itapatia kampuni ya Bw Joho karibu ukiritimba kamili zaidi ya washindani wake.

“Kutoka kiwango cha juu, mamlaka haina pingamizi kwa ombi la KR kuhusu waagizaji bidhaa kuteua moja kwa moja pamoja na kubadilisha kituo cha usafirishaji mizigo kuelekea NFT,” Alisema Bw Mwangemi.

Hata kabla ya amri hiyo kuanza kutekelezwa, wadau katika sekta ya usafirishaji bidhaa wamelalamika wakisema kuwa serikali haitapoteza mapato pekee, lakini hatua hiyo pia itawahangaisha wafanyabiashara ambao baadhi yao wana mikataba ya muda mrefu na kampuni nyinginezo za usafirishaji mizigo yao.

Mwenyekiti wa Muungano kuhusu Vituo vya Kusafirisha Kontena Nchini (CFSs) Daniel Nzeki, alisema kuwa hatua hiyo ni kinyume na jambo walilokuwa wakipigia debe akisisitiza kwamba watatetea kuwepo na usawa zaidi katika sekta hiyo.

You can share this post!

Walionufaika na kupoteza kwa uamuzi wa korti kuhusu BBI

Hofu Ulaya ikipunguza chanjo za Covid-19 Afrika