Habari Mseto

'Wadau wote sekta ya bodaboda watoe mafunzo kwa wahudumu'

February 19th, 2020 1 min read

Na DIANA MUTHEU

WADAU katika sekta ya bodaboda wameombwa kuungana na kufadhili mafunzo kwa madereva ili kupunguza visa vya uvunjaji wa sheria na kanuni za trafiki.

Akizungumza Jumatano na wanahabari katika uwanja wa mapumziko wa Uhuru Park, Nairobi, Katibu mkuu wa chama cha kuhakikisha usalama wa wahudumu wa bodaboda (BAK) Kenneth Onyango alisema kuwa wadau wengine katika sekta ya bodaboda wametelekeza hoja ya kutoa mafunzo huku chama hiki kikiachiwa majukumu yote.

“Sekta hii ina wadau wanaopata mamilioni ya pesa, lakini bodaboda wanapojikuta pabaya, ni chama tu ambacho uhusishwa,” akasema Bw Onyango.

Katibu mkuu wa chama cha kuhakikisha usalama wa wahudumu wa bodaboda (BAK) Kenneth Onyango akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi. Picha/ Diana Mutheu

Wadau waliotajwa ni pamoja na serikali, wauzaji wa pikipiki na bidhaa zake na shule za kutoa mafunzo kwa madereva.

“Wadau hawa wote wanafaa kuhofia sekta hii inapotajwa kuwa na hila nyingi kama vile wahudumu kuhusika katika wizi, mauaji ama kusababisha ajali, kwa kuwa madereva wa bodaboda wakiacha kununua pikipiki hizi, zitaenda wapi?” akauliza Bw Onyango.