Habari

Wadhamini wa shule za kimisheni Kakamega walaumiwa kuyumbisha utaratibu shuleni

July 3rd, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

[email protected]

WALIMU wakuu wa shule kadha katika Kaunti ya Kakamega wanawalaumu wadhamini wa shule za kimisheni kwa kuhujumu shughuli za kawaida na hivyo walimu kukosa muda wa kutosha kukamilisha silabasi kama inavyopendekeza Wizara ya Elimu.

Wanasema hatua hiyo inachangia kuzoroteka kwa hali ya elimu katika kaunti.

Wakuu hao wa shule kadhaa za upili waliozungumza na Taifa Leo walilalamika kwamba baadhi ya wadhamini wanachukua majukumu ya usimamizi wa shule badala ya kujikitika kwa ustawishaji wa hali ya kiroho shuleni pamoja na shughuli nyingine za kidini.

Wanasema pia vyombo hivyo vya kidini vimekuwa vikiwalazimisha wanafunzi kufanya mitihani ambayo vimeteua wataalamu wa kutunga maswali na ushindani unakuwa kwa misingi ya ushirikiano wa kidini katika kiwango cha kaunti ndogo, kaunti na hata kimaeneo.

“Kanisa Katoliki linaratibu mitihani ya kila mwaka kwa wanafunzi wa kidato cha nne na kusahihishiwa na walimu wanaofunza katika shule hizo zinazodhaminiwa na kanisa. Hali ni iyo hiyo katika shule zinazodhaminiwa na Kanisa la Anglikana,” amefichua mwalimu ambaye amesema jina lake lisichapishwe kwa sababu ya kuhofia anaweza akahangaishwa na wadhamini hao wa kidini.

Baadhi ya walimu wakuu wanasema wadhamini hao hulazimisha au hupenyeza baadhi ya watu katika bodi za usimamizi wa shule.

“Baadhi ya wadhamini hao hutaka kutumia raslimali na mali ya shule kama basi hata kwa shughuli zisizo za kielimu,” amesema mwalimu mmoja ambaye hakutaka jina litajwe.