Makala

Wafahamu mbwa bora katika shughuli za ulinzi

September 9th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MBWA wanasifiwa kutokana na majukumu yake ya kipekee katika shughuli za ulinzi.

Pia kuna wanaowafuga, hasa wale maridadi, kwa sababu ya upendo wao kwao.

Huku mbwa wakifahamika kama wanyama waaminifu kwa binadamu, wamegawanywa kwa makundi mbaimbali, kwa mujibu wa tabia, hulka na maumbile.

Wapo mbwa aina ya Golden Retriever, Rot Wailers, St Bernard, German shepherd, Caucasian Ovcharka, kati ya wengineo.

Wanaofuga wanyama hao kwa minajili ya ulinzi, huwalea kwa kuzingatia vigezo kadha wa kadha, ili waibuke bora katika kulinda. Hata hivyo, aina mbili ya mbwa, ndio; German shepherd na Caucasian ovcharka pia Caucasian shepherd au Caucasian mountain ndio maarufu katika shughuli za ulinzi.

 

Nicholas Ng’ang’a mfugaji wa mbwa. Picha/ Sammy Waweru

Nicholas Ng’ang’a ambaye ni mfugaji wa mbwa aina ya Golden Retriever, Rot Wailers na German shepherd, anasema muhimu zaidi katika ufugaji wa mbwa wa ulinzi ni uadilifu, heshima, utiifu na zaidi ya yote ni nidhamu.

“Huwafunza kwa makundi matatu, wale wa kunusa (sneaver), wa ulinzi (guard) na wa kuongoza (guide),” Ng’ang’a ambaye alianza ufugaji wa mbwa mwaka wa 2009 anafafanua.

German shepherd ni aina ya mbwa wanaotajwa kuwa jasiri katika ulinzi na pia werevu. Salome Nyambura ni mfugaji mwingine wa mbwa wa ulinzi. Mwanadada huyo hufuga mbwa aina ya German shepherd na Caucasian Ovcharka.

Salome alianza na St Bernard, anayemtaja kwamba amesheheni hulka za upole, rafiki na anayesifiwa kuwa ngangari katika ulinzi.

Caucasian Ovcharka ndiye bora zaidi katika ulinzi. “Ni mbwa jasiri na anapokomaa, huwa na uzani wa zaidi ya kilo 100,” mfugaji huyo anaelezea.

Isitoshe, Salome anasema ni mbwa wa hadhi yake na anayehitaji mafunzo ya hali ya juu. “Unapotembea na Caucasian shepherd unahisi kweli una mbwa wa aina yake. Ni maumbile yanayomfanya kuwa bei ghali,” anasema.

Mbwa hulishwa chakula maalum aina ya Skinners, Royal Canin na pia Happy dogs. Vilevile, hulishwa punje za mchele na nyama ya mifugo na kuku. Usafi wa lishe na makazi ya mbwa unapaswa kuwa wa hali ya juu, ili kuzuia maambukizi ya maradhi na kuwepo kwa vimelea.

Ufugaji wa mbwa wa ulinzi ukikumbatiwa ni biashara inayoweza kukuingiza mapato ya kuridhisha, ikizingatiwa kuwa ni shughuli isiyofanywa na wengi.