Habari Mseto

Wafanyabiashara Mtito Andei waumia

May 16th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WAFANYABIASHARA katika eneo la Mtito Andei katika barabara kuu ya Mombasa kuelekea Nairobi wanasema wanaendelea kukadiria hasara kubwa kufuatia kufungwa kwa kaunti za Mombasa, Kwale, na Kilifi.

Aidha zaidi ya wafanyabiashara 500 wanaofanya biashara mbalimbali ikiwemo kwenye mikahawa, vituo vya mabasi, wauzaji wa asali na bidhaa zingine walisema wanaendelea kukadiria hasara baada ya janga la Covid-19 kufanya shughuli nyingi kukwama.

Serikali ilifunga kaunti ya Mombasa ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Kaunti ya Mombasa ndiyo kitovu cha biashara mbalimbali za Pwani ikiwemo bandari, utalii na uchukuzi.

Lakini tangu kaunti hiyo ifungwe, hakuna biashara zinazoendelea kaunti zinazotegemea Mombasa kwa biashara hususan uchukuzi.

“Kabla ya janga hili biashara ilikuwa inanoga lakini kwa sasa hakuna lolote, hoteli imekuwa kama uwanja wa kandanda bila wachezaji na mashabiki. Tunaomba Mungu na pia serikali itusaidie kwa sababu watu wanaweza kufa njaa. Hakuna malori, mabasi wala magari ya masafa marefu,” alisema mfanyabiashara Bw Mohammed Adan akiwa kwenye mkahawa wake ulioko Mtito Andei.

Alisema wafanyakazi wake wakiwemo wasafishaji, wapishi na wahudumu wa hoteli yake wamesafiri makwao kutokana na na kuzorota kwa biashara.

Alisema maduka machache ndiyo yaliyosalia wazi lakini hakuna wateja.

Kwa siku alikuwa anahudumia wateja zaidi ya 200 lakini kwa sasa madereva wa lori wawili ndio wateja anaowauzia.

Mwingine naye akasimulia hali ilivyo.

“Kufungwa kwa hii barabara kuu ya Mombasa kuelekea Nairobi kumetuathiri. Hatuna vyakula wala kazi na hata tunaweza tukafa njaa. Tunaomba serikali ifungue biashara zetu,” alisema mfanyabiashara mwingine Bw Joshua Mwange.

Bw Mwange ambaye anafanya kazi katika kituo cha mafuta huko Mtito Andei alisema kunywea kwa sekta ya utalii kumezorotesha biashara zao.

Mtito Andei huwa ni eneo lililo karibu na mbuga ya wanyama ya Tsavo Mashariki.