Habari Mseto

Wafanyabiashara wa Kwale wanaotegemea Kongowea wataka serikali iwatambue 'watoaji huduma muhimu'

May 11th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

WAFANYABIASHARA kutoka Kaunti ya Kwale wanaotoa bidhaa zao katika soko la Kongowea mjini Mombasa, wameitaka serikali iwatambue kama wanaotoa huduma muhimu ili kuwawezesha kufikia soko hilo bila pingamizi.

Wakiongea na Taifa Leo wafanyabiashara hao wanaouza mboga maeneo ya Ibiza Ukunda, walisema Jumapili tangu kuwekwa marufuku ya kuingia na kutoka katika Kaunti ya Mombasa biashara zao zimeathirika pakubwa.

Muuzaji mboga na matunda Bw Moses Karanja alisema tangu kuwekwa kwa marufuku hayo, biashara zao zimeathirika kwa sababu wanashindwa kusafiri hadi Kaunti ya Mombasa kupata bidhaa.

“Tunaouza rejareja tumeathirika sana; kupata bidhaa imekuwa vigumu na tunaomba serikali itufikirie,” akasema.

Bw Karanja alisema kabla ya marufuku alikuwa akisafiri hadi Mombasa kununua bidhaa.

Aidha, alisema kafyu nayo imepunguza muda wa kufanya biashara zao, kwani imekuwa vigumu kufanya biashara hizo nyakati za usiku, hivyo wanazidi kupata hasara.

“Tulikuwa na matumaini, kuwa tukimaliza muda uliyowekwa na serikali mambo yatarudi kuwa kawaida, tulishtuka kumsikia Rais Uhuru Kenyatta akiongeza siku 21 zaidi,” akasema Bw Karanja.

Muuzaji mwingine Bw Edwin Otieno alipinga kuongezwa kwa muda wa marufuku kwa kutaja kuwa serikali imeshindwa kuweka mipangilio mwafaka ya kusaidia wananchi kimaisha, hali ambayo inawafanya Wakenya kukaidi marufuku yanayowekwa na serikali ili waweze kujitafutia lishe.

Bw Otieno alisema kwa sababu ya kupungua kwa bidhaa kufuatia marufuku, wanalazimika kuuza zilizoko kwa bei ya juu.

“Hali ya uchumi imekuwa mbaya kwa kila mtu na huku kupandisha kwetu bei kunafanya watu wengi washindwe kununua hivyo tunaambulia pakavu,” akasema.

Alisema kwa sasa wanauza kreti kubwa ya viazi kwa Sh800 badala ya Sh500 ambazo ni bei waliozoea wateja.