Habari Mseto

Wafanyabiashara wa ngono wakerwa na matamshi ya mbunge kuhusu huduma za Sh20

January 14th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI 

MUUNGANO wa wafanyabiashara wa ngono eneo la katikati mwa nchi (CRCSWA) umemkemea mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua kufuatia madai yake kwamba kuna kipimo cha mahaba kwa bei ya Sh20.

Wameteta kwamba matamshi hayo yalilenga kuwadunisha, kuwadharau na kuwaharibia soko.

Akiongea Mjini Thika Mnamo Januari 12, 2024 mshirikishi wa vibiriti ngoma hao Bi Esther Nyawira alilalama kwamba “hata sisi tungetaka utuonyeshe ambako mahaba hupimwa kwa Sh20”.

Aliteta kwamba “huenda mbunge huyu anajua soko hilo la Sh20 na anafaa aje tushirikiane ili tufike huko kuwaokoa wenzetu waache kunyanyaswa na wateja”.

Bi Wa Maua akiwa katika jela la Maranjau lililoko Maragua mnamo Januari 7, 2024 katika hafla ya kutuza mahabusu mlo wa mchele na nyama chini ya udhamini wa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, aliwataka wanaume kukoma kubaka wasichana.

“Badala ya kubaka wasichana katika jamii na kuishia kutupwa korokoroni afadhali uingie mtaani ujipe mahaba kwa bei ya Sh20. Huo mtindo wa kubaka wasichana ukome kwa kuwa umekuwa mwingi sana eneo hili,” akasema.

Bi Nyawira alishikilia kwamba “matamshi ya Bi Wamaua yalikosa busara kwa kuwa licha ya kwamba hata sisi tunakemea ubakaji, haikustahili kamwe aelekeze wabakaji kwa kazi yetu”.

Alisema kwamba “kuwatuma wabakaji kwetu akijua kwamba wao ni majambazi na kisha kuwachochea wawe wakitulipa Sh20 kando na kuhatarisha maisha yetu pia ni ishara ya maongezi ya ovyo ambayo huathiri sana wanasiasa tulio nao kwa sasa”.

Bi Nyawira aliwataka wafanyabiashara wote wa ngono wachukue tahadhari na wasidhubutu kuhudumia wateja ambao watasikika wakirejelea matamshi ya Bi Wamaua kuhusu bei.

“Hakuna sheria ambayo inampa mbunge mamlaka ya kuweka bei ya mahaba hapa nchini. Yeye aende akatetee bei za mafuta ambazo hutangazwa kila tarehe 15 ya mwezi. Mahaba sio mafuta au basari. Wamaua azingatie yanayomhusu,” akasema.

Alishikilia kwamba kwa sasa bei ya chini zaidi ya mahaba ni Sh300 kwa chini ya dakika 10.

“Bi Wamaua anafaa aandae kikao cha uhamasisho kuhusu ukahaba kwa kuwa katika eneobunge lake pekee tuna wanachama 1,328 ambao hutoa huduma zao katika miji mbalimbali, wengine wengi wakiwa bado hawajajisajili na sisi,” akasema.

Aliongeza kwamba “ukahaba kwa kiwango kikuu ni sekta ya waliodunishwa na maisha na badala ya kungojea umasikini uwaue au uwatwike aibu ya kutojiweza, wakaingia katika safu hiyo bado wakiwa na matumaini ya kujiondoa”.