Habari Mseto

Wafanyabiashara wanawake wawanyooshea kidole cha lawama maafisa wa usalama Garissa

June 5th, 2020 1 min read

Na FARHIYA HUSSEIN

WANAWAKE zaidi ya 50 waliandamana Alhamisi katika Kaunti ya Garissa wakilalamika kuwa maafisa wa usalama wanaua biashara zao kwa kuteketeza na kuharibu bidhaa zao wakisema ni za magendo.

Wanawake hao walishutumu maafisa hao wa usalama – wakiongozwa na Kamishna wa Kaunti – kwa kile walitaja ni kuchukua uamuzi wa kuharibu bidhaa zao bila kuwataarifu wamiliki.

Bi Dahabo Abdi ambaye bidhaa zake ziliharibiwa alisema haikuwa mara ya kwanza kufanyiwa hivyo.

“Miezi kadhaa iliyopita waliwasha moto lori langu la kubeba mizigo,” alisema.

Mwenzake, Bi Hafsa Ali anasema wamepoteza zaidi ya Sh6 milioni kutokana na operesheni ya wiki iliyopita na kuwasihi viongozi wa serikali waache kuharibu bidhaa bila idhini kutoka kwao kwani hii itawafanya kukosa kazi.

“Tulinunua nafaka kutoka upande wa Dadaab; hii imekuwa njia yetu ya kuishi kwa miongo kadhaa sasa,” alisema Bi Ali.

Akiongea ofisini kwake, Mshirikishi wa Kaskazini Mashariki, Nick Ndalana alisema wanawake hawakuthibitisha bidhaa zilikuwa mali yao halali.

“Hakujakuwa na mawasiliano yenye ufanisi na tunaendelea kulifuatilia hili suala,” alisema.

Bw Ndalana alisema wana sababu zote za kuamini kwamba mchele ambao ulikuwa ukisafirishwa katika malori ni bidhaa za magendo na hilo halitakubalika.

Wiki iliyopita walinda usalama walinasa mifuko yenye bidhaa ikisafirishwa kwa malori kutoka Dadaab. Mali hiyo ilitwaliwa na kuharibiwa.