Habari Mseto

Wafanyabiashara wanne washtakiwa kuiba dizeli ya Sh13.5m

January 24th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

WAFANYABIASHARA wanne wa kuuza bidhaa za petroli, wameshtakiwa kwa wizi wa lita 70,000 za dizeli ya thamani ya Sh13.5 milioni.

Mabw Douglas Macharia Maina, Dominc Kimotho, Evans Njuguna Mweha, na Lewis Musau Masaku, walikana mashtaka ya kula njama kuiba mafuta, wizi wa lita 70,000 za dizeli na kupatikana wakiuza mafuta hayo ya dizeli wakijua yaliibwa ama kupatikana kwa njia isiyo halali.

Wanne hao walidaiwa kwamba walikula njama za kuiba mafuta hayo kati ya Novemba na Desemba 2023.

Mashtaka ya pamoja dhidi ya washtakiwa hao yalikuwa ya kula njama za kuiba na wizi wa lita za mafuta ya dizeli kati ya Novemba 23 na Desemba 20, 2023.

Upande wa mashtaka uliongozwa na wakili wa serikali Bw James Gachoka aliyemweleza hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bernard Ochoi kuwa washukiwa hao walishirikiana na watu wengine wanaoendelea kusakwa na polisi wakitekeleza wizi huo.

Mahakama ilielezwa thamani ya mafuta yaliyoibwa ni Sh13,580,000.

Wanne hao, mahakama iliambiwa, waliiba mafuta hayo kutoka Petro City Energy (K) Limited.

Bw Maina alishtakiwa kivyake kwamba alipatikana akiwa amehifadhi lita 30,000 za dizeli ya thamani ya Sh5.8 milioni katika kituo cha kuuzia mafuta cha 360 Energy Komarock Petrol Station.

Shtaka lilisema alijua mafuta hayo yalikuwa yameibwa au kupatikana kwa njia isiyo halali.

Naye Bw Kimotho, mahakama ilielezwa kwamba polisi walimpata akiwa amehifadhi lita 10,000 za dizeli yenye thamani ya Sh1,940,000 katika kituo cha petroli cha Trojans Petrol Station kilichoko eneo la Kiboko, Kaunti ya Makueni mnamo Desemba 20, 2023.

Shtaka lilisema alijua mafuta hayo yalikuwa yameibwa au kupatikana kwa njia isiyo halali.

Nao Mabw Mweha na Masaku walishtakiwa kwa kupatikana wakiwa wamehifadhi lita 10,000 za dizeli ya thamani ya Sh1,940,000 katika kituo cha kuuzia mafuta cha Industrial Area Deport.

Walikana kwamba walijua mafuta hayo yalikuwa yameibwa.

Mawakili Nahashon Kanyi, Shadrack Wambui, na Mitchell Omwoyo waliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana.

Bw Wambui alieleza korti kwamba washtakiwa ni wafanyabiashara na kwamba kazi zao zimeathirika pakubwa kufuatia kutiwa nguvuni kwao.

Bw Gachoka hakupinga ombi la washtakiwa hao kuachiliwa kwa dhamana akisema walikuwa nje kwa dhamana ya polisi.

Bw Ochoi aliamuru kila mmoja alipe dhamana ya pesa taslimu Sh500,000.

Kesi itatajwa Februari 7, 2024.