Habari za Kaunti

Soko la Kwa Jiwa lasalia mahame wafanyabiashara wakilalamikia mazingira duni

January 27th, 2024 2 min read

NA ALEX KALAMA

SOKO la Kwa Jiwa lililoko katikati ya mji wa Malindi lilisalia mahame mnamo Ijumaa baada ya wafanyibiashara wa soko hilo kudai kupuuzwa na serikali licha yao kulipa ushuru kila siku.

Licha ya wafanyabiashara hao kufanya mkutano na maafisa wa serikali ya Kaunti ya Kilifi, wanasisitiza haja ya kushughulikiwa kwa matakwa yao, ikiwemo soko hilo kuwekwa umeme, maji safi na usafi wa soko hilo kudumishwa.

Wakihutubia na wanahabari mjini Malindi, wafanyabiashara hao wakiongozwa na Bi Furaha Robert walisema hali ya usafi wa mazingira katika soko hilo ni mbaya mno na licha ya kutoa malalamiko yao kwa serikali ya kaunti, bado kilio chao kimepuuzwa.

“Mimi nafanya biashara katika soko hili lakini usafi umezorota licha ya sisi kulipa ushuru,” akasema Bi Robert.

Aliongeza kwamba wakati wa mvua, wafanyabiashara na wateja wao hunyeshewa.

“Halafu vyoo ni vichafu. Choo kimoja kinatumika kwa wanawake na wanaume vile vile. Kwa choo tunalipa Sh10 mtu akiingia lakini hizo pesa hatujui zinafanyiwa nini maana vyoo kwa kweli havioshwi,” akalalamika.

Kwa upande wake Bw Elisha Odima, anahofia kuzuka kwa maradhi kama vile kipindupindu huku akieleza kuwa tayari ugonjwa wa macho kuwa mekundu unaoshuhudiwa katika eneobunge la Malindi tayari umewaathiri baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo.

“Kwa hivyo ukiona hapa sokoni kila mmoja amevaa miwani hata ambao huwa hawavai, ni kwa sababu ya ugonjwa wa macho. Ikiwa ni kweli kuwa uchafu huusambaza, tuko kwa hatari kubwa ya kuupata kwa sababu hapa sokoni kuna rundo la taka,” akasema Bw Odima.

Mfanyabiashara Elisha Odima akiwa katika soko la Kwa Jiwa mjini Malindi mnamo Januari 26, 2024. PICHA | ALEX KALAMA

Alisema kwa sababu ya taka hizo, mabuu hutembea yakija mahali pa kuuzia chakula.

“Kando na ugonjwa wa macho, kipindupindu pia kinaweza kutokea wakati wowote na kikija pale kitaramba wengi sana,” akasema.

Naye mwenyekiti wa bodaboda katika eneobunge la Malindi Jackson Thoya ambaye pia ni mfanyabiashara katika soko hilo, alisema wamekuwa wakitozwa ushuru wa hali ya juu zikiwemo siku za Jumamosi na Jumapili na wakati mwingine wakilazimika kusafisha soko hilo wenyewe.

“Hao Jumamosi wako pale saa kumi na moja asubuhi wanakata ushuru, Jumapili wako pale wanakata ushuru na tukiwauliza ‘tunajua kwa kaunti ofisi zinafungwa Ijumaa jioni, hivyo Jumamosi na Jumapili mnatakaje?’ wanasema ni lazima tukate, eti wametumwa na wakubwa,” akasema Bw Thoya.

Alisema wasipolipa Jumamosi na Jumapili hufurushwa sokoni.

Soko la Kwa Jiwa mjini Malindi ambalo limesalia mahame baada ya wafanyabiasha wengi kufunga biashara zao mnamo Januari 26, 2024, wakilalamika kwa kupuuzwa na serikali ya kaunti ya Kilifi licha ya kutoa ushuru kila siku. PICHA | ALEX KALAMA