Habari Mseto

Wafanyakazi 2 wapatikana na hatia ya wizi wa Sh20m za mikopo kwa wakulima

May 28th, 2024 1 min read

NA TITUS OMINDE

WAFANYAKAZI wawili wa Shirika la Kutoa Mikopo kwa Wakulima Kilimo (AFC) tawi la Eldoret ambao wamepatikana na hatia ya kuiba zaidi ya Sh20 milioni za mwajiri wao wako katika hatari ya kufungwa jela kwa muda usiozidi miaka sita.

Mnamo Jumatatu, Hakimu mkuu wa Eldoret Dennis Mikoyan aliwapata Vincent Rotich na Rose Cheboi na hatia ya kuibia mwajiri wao.

Wawili hao walishtakiwa kwa mashtaka 10 ya wizi na kughushi hati ambazo walitumia kuibia mwajiri wao.

Shtaka la kwanza lilisema katika tarehe tofauti kati ya Oktoba 2016 na Septemba 2018, washtakiwa pamoja na wengine ambao hawakufika mahakamani, waliiba Sh3,715,500 kutoka kwa akaunti wamiliki wa akaunti mbalimbali katika benki ya AFC tawi la Eldoret.

Katika shtaka la pili Rose Cheboi alishtakiwa kwa kuiba Sh3.7 milioni katika tarehe tofauti kati ya Septemba 12 na Septemba 28, 2017.

Mahakama iliambiwa kwamba Cheboi pamoja na wengine ambao hawakufika mahakamani waliiba pesa ambazo alizipata kama mfanyakazi na karani wa fedha katika AFC.

Rotich pamoja na wengine ambao hawakufika mahakamani walishtakiwa kwa kuiba Sh11.3 milioni ambazo alizipata akiwa mfanyakazi wa AFC.

Kulingana na hati ya mashtaka aliiba pesa hizo kwa tarehe tofauti kati ya Aprili 2016 na Machi 19, 2018.

Vilevile walishtakiwa kwa mashtaka mbalimbali ya kughushi nyaraka ambazo walitumia kuiba kutoka kwa akaunti za wateja wa AFC zaidi ya Sh5m kwa tarehe tofauti kati ya 2016 na 2018.

Walikuwa wamekanusha mashtaka walipofikishwa mahakamani Oktoba 31, 2018.

Mahakama iliwaachilia kwa dhamana.

Watahukumiwa Juni 25, 2024, baada ya kupatikana na hatia ya mashtaka yote 10.