Habari Mseto

Wafanyakazi 4,000 wakubaliwa kumshtaki kinara wa RBA

January 23rd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYAKAZI 4,000 wa zamani wa Shirika la Posta na Simu (PCK) Jumatano walikubaliwa na mahakama kuu wamfungulie mashtaka kinara wa mamlaka ya malipo ya uzeeni RBA Bw Nzomo Mutuku kwa kukaidi amri afanye hesabu ajue wanastahili kulipwa pesa gapi za malipo yao ya uzeeni.

Naibu wa msajili wa mahakama kuu alimruhusu wakili Titus Koceyo awasilishe kesi akiomba Bw Nzomo Mutuku akamatwe na kutupwa jela kwa kukaidi maagizo ya Jaji George Odunga ya Februari 22, 2018.

Jaji Odunga alimwamuru Bw Mutuku awasiliane na maafisa wahusika katika PCK kufanya hesabu ya pesa ambazo kila mmoja wa wafanyakazi hao 4,000 wa PCK waliostaafishwa anapasa kulipwa kama malipo ya uzeeni.

Jaji huyo alikuwa amempa muda wa siku 60 kufanya hesabu ajue malipo ya kila mmoja.

Bw Koceyo alisema kufikia sasa Bw Mutuku hajafanya hesabu hiyo.

Wakili huyo aliambia mahakama muda wa siku 60 ulikamilika Aprili 22 mwaka uliopita na miezi sita tayari imeisha na “ bado Bw Mutuku hajafanya hesabu hiyo.”

Mahakama ilifahamishwa kuwa wafanyakazi hao waliostaafishwa wanakumbwa na shida mbali mbali na iwapo mahakama haitamchukulia hatua Bw Mutuku wataendelea kutaabika.

Mahakama ilifahamishwa Bw Mutuku amezebea kutekeleza majukumu yake.

“Naomba hii mahakama  iwaruhusu walalamishi wamshtaki Bw Mutuku kwa kukaidi maagizo ya Jaji Odunga kwamba afanye hesabu ya pesa wanazostahili kulipwa,” alisema Bw Koceyo.

Wakili huyo alisema lazima maagizo ya korti yatekelezwe.

“Ikiwa maagizo ya hii mahakama yatakaidiwa basi nchi hii itakuwa haitawaliki,” alisema Bw Koceyo.

Mahakama ilikubalia ombi hilo la Bw Koceyo na kuamuru kesi hiyo isikizwe Feburuari 7, 2019.