Habari Mseto

Wafanyakazi hewa na wasiofika kazini kupokea mishahara hewa

December 10th, 2018 1 min read

NA DAVID MUCHUI

WAKUU wa Idara mbalimbali katika serikali ya Kaunti ya Meru watatakiwa kuandaa orodha ya wafanyakazi wanaoripoti kazini, hii ikiwa njia ya uongozi wa Gavana Kiraitu Murungi kuondoa wafanyakazi ghushi na wale wasioripoti kazini.

Akizungumza wakati wa sherehe za mwisho wa mwaka kwa wafanyakazi wa kaunti hiyo ugani Kinori mnamo Jumamosi, Naibu Gavana Titus Ntuchui alionya kwamba watahakikisha mfanyakazi atakayekosa kufika kazini ataondolewa katika orodha ya wanaolipwa mishahara.

“Tutakuwa tunaandaa orodha ya wanaofika kazini kila mwezi kwa kila idara na yeyote atakayekosa kukamilisha siku zake za kuwa kazini ataondolewa kwenye listi hiyo. Hatutaki kupoteza fedha za umma kuwalipa wafanyakazi wasiowajibika,” akasema Bw Ntuchui.

Aidha, kiongozi huyo alisema kwamba orodha hiyo pamoja na kutiwa saini kwa mikataba ya kufanya kazi itachangia wafanyakazi kukaza kamba katika kuhakikisha masuala yaliyo kwenye manifesto ya Gavana yanatekelezwa.

“Tumeanza kutia saini mikataba kwa wafanyakazi wetu. Kwa kutumia mikataba hiyo tutaorodhesha idara zote na kutunuku zile zinazong’aa kisha kukemea na kuzionya zinazozembea,” akaongeza Bw Ntuchui. Awali Bw Murungi alifichua kwamba serikali yake itamakinikia kuwang’oa wafanyakazi wanaofika kazini kisha kuangika makoti yao kwenye viti na kuyoyomea nje kazi zao za kibinafsi.

Gavana huyo vile vile alitaja ufanisi aliojivunia kwa kipindi cha mwaka moja uliopita. Baadhi ya miradi aliyofanikisha ikiwa ni uchimbaji wa visima 100, kusajili vijana 1000 katika Shirika la Huduma kwa vijana wa Meru(MYS) na maziwa ya bure kwa wanafunzi wa shule zote za chekechea kwenye kaunti hiyo.