Habari Mseto

Wafanyakazi kaunti zote waunda chama cha kujitetea

April 8th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

WAFANYAKAZI wa kaunti zote nchini wameunda muungano wa kikazi wa kuwatetea kutokana na kudhulumiwa kikazi na kupigwa kalamu kila mara na magavana, haswa baada ya uongozi unapobadilishwa.

Wafanyakazi hao wameunda muungano huo wakati serikali nyingi za kaunti zikiwa na migogoro na wafanyakazi wake ambao waliajiriwa na magavana wa awali waliobwagwa uchaguzini, mingi ikiishia kortini.

Muungano huo, Kenya County Administrators Union (KCAU) sasa unatarajiwa kuleta suluhu ya kudumu kwa wafanyakazi wa kaunti wanaosimamia wodi, kaunti ndogo na usimamizi mwingine ambao wamekuwa wakihangaishwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari walipozindua muungano huo katika hoteli ya Nuru Palace mjini Nakuru siku ya Ijumaa, viongozi wa muungano huo walisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na wakati wa kubadilishana hatamu za uongozi tangu uchaguzi wa Agosti mwaka uliopita, kumekuwa na migogoro mingi ya kikazi na wafanyakazi wengi kupigwa kalamu.

Walisema kuwa japo wafanyakazi hao wanaajiriwa kwa kufuata sheria na kuwa wamefuzu katika taaluma wanazofanya kazi, viongozi wa kaunti wamekuwa na hulka ya kuwafuta bila kufuata sheria ila kwa misingi ya siasa tu.

Viongozi zaidi walitaja mizozo baina ya wafanyakazi na serikali za kaunti za Bomet, Pokot Magharibi, Nakuru na Taita Taveta kama mfano wa namna wafanyakazi wamehangaishwa kwa misingi ya kisiasa pekee.