Habari za Kaunti

Wafanyakazi wa kiwanda cha korosho wadai haki kabla ufufuzi

May 26th, 2024 2 min read

NA MAUREEN ONGALA

HUKU serikali ikinuia kufufua kiwanda cha korosho mjini Kilifi, maelfu ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho waliandamana wakiishinikiza kuingilia kati ili waweze kupata pensheni na marupurupu yao ambayo wamekuwa wakidai tangu kufungwa kwa kiwanda hicho.

Wafanyakazi hao walipiga kambi nje ya lango la kampuni hiyo wakiwa na matumaini ya kuwa siku moja watapata haki yao.

Kulingana na wafanyikazi hao, licha yao kufuata mkondo wa sheria kudai mamilioni ya pesa zao, kesi iliyoko mahakamani imekwama, mhusika mkuu akikosa kupatikana.

Wakiongozwa na katibu wa muungano wa wafanyakazi hao wa korosho Bw Douglas Katana, wazee hao waliitaka serikali kuingilia kati ili wapokee pesa wanazodai.

Mzee Katana,74, ambaye ndiye kiongozi wa pekee amesalia kati ya wazee walioanzisha safari ya kupigania haki yao, alielezwa wasiwasi wake kuwa huenda wafanyakazi hao wakakosa kupata malipo yao kwani tayari wengi wameaga dunia.

“Wenzangu walishaaga dunia na leo mimi nikifa pesa hizi zitapotea na sitaki hilo litendeke. Matumaini yangu ni kwamba pesa zitatoka mapema kwa sababu wazee na familia zao wanufaike kutokana na jasho lao,” akasema Bw Katana.

Naye Bi Hilda Mzungu, ambaye pia anaishi na ulemavu mjini Kilifi, alitaka serikali kuingilia kati kuwalipa marupurupu yao kabla ya kufufua kiwanda cha kuchakata korosho mjini humo.

Bi Mzungu alieleza kuwa aliajiriwa katika kiwanda hicho cha kuchakata korosho akiwa na umri wa miaka 19 na alifanya kazi hadi kilipofungwa.

“Tulifutwa kazi ghafla na tulitoka hapo na Sh100 ambazo zilikuwa karadha ya mshahara wetu na tangu hapo, tumekuwa tukiteseka. Mimi licha ya ulemavu ninalazimika kufanya kazi ya mjengo, kubeba mawe na simiti. Serikali isifungue kiwanda hicho kabla ya kutupa pesa zetu,” akasema Bi Mzungu.

Mzee mwingine, Bw Katana Kazungu alielezea kughadhabishwa kwake na jinsi walivyonyanyaswa, hatua ambayo alisema ilileta changamoto nyingi katika maisha yake.

Alisema kuwa wafanyakazi hao walifutwa siku moja tu baada ya kulipwa mshahara.

Wakili Dennis Kinaro alimwandikia Mwanasheria Mkuu nchini kumtaka aingilie kati na kuhakisha wafanyakazi hao wanalipwa pesa zao.

Kulingana na wakili Kinaro, imekuwa vigumu kwa wafanyakazi hao kulipwa, akidai maafisa wakuu waliochukua uongozi wa kampuni hiyo walidinda kuzungumza naye kutafuta muafaka.

[email protected]