Habari Mseto

Wafanyakazi wa KQ watisha kugoma safari za Amerika zikikaribia

October 23rd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Huku zikiwa zimesalia siku chache kabla ya Shirika la Ndege la Kenya Airways (KQ) kuanza safari ya moja kwa moja hadi Marekani, wafanyikazi wake wametoa notisi ya kugoma.

KQ itaanza ziara hiyo Oktoba 28, 2018, safari itakayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Jumatatu, wahudumu, kupitia kwa chama chao waliahidi kwenda mgomo baada ya shirika hilo kushindwa kukubaliana nao mshahara maalum na kuimarisha mazingira ya ufanyikazi kwa wahudumu wa ziara za masafa marefu.

Kulingana na chama hicho (KAWU) hatua watakazochukua zitakuwa ni pamoja na wahudumu wa Boeing 787 Dreamliner kukataa kufanya kazi siku ya kwanza katika ziara ya moja kwa moja kuelekea Marekani.

Wahudumu wa uwanjani hata nao wanatarajiwa pia kugoma siku hiyo. Zaidi ya mshahara mzuri kwa wahudumu wa Boeing 787 Dreamliner, chama hicho kinataka kukamilishwa kwa mkataba wa makubaliano ya mishahara na marupurupu (CBA) ambao umekuwa ukijadiliwa kwa muda mrefu.

“Tunataka usimamizi kukamilisha majadiliano ya CBA kabla ya Oktoba 28,” alisema Katibu Mkuu wa KAWU Moses Ndiema, Oktoba 17 katika barua aliyoandikia wasimamizi na wahudumu wa KQ.

“Tangazo hili ni kwa wahudumu wetu wote katika idara zote kujiepusha na ziara ya Marekani mpaka chama kitoe ushauri,” alisema katibu huyo.

Hata hivyo, mkurugenzi mkuu Sebastian Mikosz aliwaomba kukomesha mpango wa mgomo kwa kuwaahidi kujadiliana nao kuhusu CBA baada ya uzinduzi wa safari hiyo.

Licha ya chama hicho kutaka wahudumu kulipwa Sh20,000 kwa kila saa zaidi ya muda wa kawaida, KQ ilitoa ofa la kulipa Sh5,000 kwa saa moja.