Wafanyakazi walioangukia ‘manna’ waamrishwa wairejeshe

Wafanyakazi walioangukia ‘manna’ waamrishwa wairejeshe

Na GEORGE ODIWUOR

WAFANYAKAZI 3,000 wa Kaunti ya Homa Bay walipigwa na butwaa baada ya kulipwa mshahara wa Sh0 huku wenzao wakipata ‘nyongeza’ ya asilimia 200 ya mishahara yao.

Wafanyakazi ambao huwa wakilipwa Sh30,000, kwa mfano, walipata mshahara wa Sh150,000. Serikali ya Kaunti sasa imewataka wafanyakazi waliolipwa ‘mshahara mnono’ warejeshe sehemu ya fedha hizo huku ikisema kuwa palikuwa na hitilafu katika mfumo wa malipo ya mishahara ya Juni.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Wafanyakazi, Omondi Auma alisema kuwa hitilafu hiyo ilitokea katika benki mbili.

Bw Auma amewatumia barua wafanyakazi wote akiwataka waliopata fedha zaidi katika mishahara yao kuzirejesha mara moja.

Alisema kuwa wafanyakazi watakaokataa kurejesha fedha hizo wataandikiwa deni na kukatwa mishahara yote kuanzia mwezi ujao hadi wamalize kulipa.

“Lengo la barua hii ni kuwasihi waliopokea mishahara mikubwa kuliko kawaida, kuzirejesha pesa za ziada katika akaunti ya benki ya serikali ya Kaunti ya Homa Bay na kisha wapeleke risiti kwa meneja wa mishahara. Watakaokataa kuzirejesha wataandikiwa deni na kuanzia mwezi huu watakatwa mishahara yao yote hadi pale watakapomaliza kulipa,” akasema.

Baadhi ya wafanyakazi waliambulia patupu kwani walipokea mishahara sufuri huku wengine wakipata nusu.

Serikali ya kaunti hiyo imewataka wafanyakazi ambao hawakupata mshahara na wale waliopata fedha ndogo kuwa wavumilivu kwani watapokea mishahara ya miezi miwili Agosti.

Serikali ya Kaunti pia ililazimika kuwaomba msamaha wafanyakazi walioambulia patupu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali tawi la Homa Bay, Tom Akech alisema kuwa wafanyakazi 3,000 walilipwa Sh0 na hao ndio walioanza kulalamika baada ya kuona wenzao wakisherehekea.

“Nilipokea malalamishi kwamba mishahara ya Juni ilicheleweshwa. Baadaye ilibainika kuwa waliokuwa wanalalamika hawakupata mshahara na wenzao walikuwa wamelipwa fedha nyingi kuliko kawaida,” akasema Bw Akech.

Alisema hitilafu hiyo imesababisha wasiwasi miongoni mwa wafanyakazi waliokosa mishahara yao.

“Mishahara ya wafanyakazi wa serikali ya Kaunti ya Homa Bay imekuwa ikicheleweshwa mara kwa mara na sasa mitambo ina hitilafu,” akasema.

Wafanyakazi wamepanga maandamano wiki hii hadi kwa afisi ya Gavana Cyprian Awiti kuwasilisha malalamishi yao.

Bw Akech alisema kuwa wafanyakazi wa kaunti wamechoshwa na kucheleweshwa kwa mishahara yao kila mwezi.

You can share this post!

360 Media yatua kileleni, Makarios, Leopards zikiteleza

Raila ataja sera atakayofuata akiibuka mshindi mwaka 2022