Habari Mseto

Wafanyakazi watapoteza kazi wakikatwa ada ya nyumba – Waajiri

June 22nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Waajiri wameonya kuwa huenda wafanyakazi wengi wakapoteza kazi ikiwa serikali itatekeleza pendekezo la kukata asilimia 0.5 ya mshahara kufadhili hazina ya nyumba.

Kulingana na waajiri hao, hatua hiyo itazidisha gharama ya kufanya biashara na kuwapunguzia wafanyikazi mapato yao.

Kulingana na pendekezo hilo, waajiri na waajiriwa watakatwa hadi Sh5, 000 kufadhili mradi huo.

“Mapendekezo hayo yatazidisha gharama ya leba kwa waajiri na gharama ya maisha kwa wafanyikazi ambao hawajui jinsi mpango huo utakavyowafaidi,” alisema Rais wa Shirikisho la Waajiri (FKE) Mark Obuya Alhamisi.

Kwa sasa, waajiri huwalipia wafanyikazi Sh200 kufadhili Hazina ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF).

Ikiwa pendekezo hilo litapitishwa, wafanyikazi wote ambao wanapata Sh100, 000 watachanga Sh500 kwa mwezi kufadhili mradi huo.

Pendekezo hilo linatarajiwa kuwaathiri vibaya zaidi wafanyikazi wanaopata chini ya Sh50, 000.