Wafanyibiashara walia kukosa biashara kituo cha mizigo cha Naivasha

Wafanyibiashara walia kukosa biashara kituo cha mizigo cha Naivasha

NA BRIAN WASUNA

HATUA ya Rais William Ruto kuhamisha shughuli za kupakua mizigo kutoka kituo cha makonteina (ICD) cha Naivasha hadi Mombasa, imeathiri wafanyabiasha wadogo eneo hilo.

Wafanyabiashara wanaouza bidhaa za duka kama vile maziwa, sukari, unga, mafuta na maji ya chupa karibu na kituo hicho kilichoko Suswa, sasa wanalalamika kupata hasara baada ya wateja kupungua.

“Biashara ilikuwa nzuri hadi juzi ambapo Rais Ruto alitoa amri kwamba shughuli za bandari zirejeshwe Mombasa. Sasa nimesalia na mrundiko wa bidhaa na sijui la kufanya. Ni malori machache mno yanayoingia na kutoka kituo cha ICD. Hata watalii wamepungua kwa kiwango kikubwa mno,” akasema Beatrice Rioba anayeendesha biashara ya kioski.

Mnamo Julai 2021 Bi Rioba, ambaye alikuwa akiendesha biashara mjini Nakuru, alihamia eneo la Suswa na kuanzisha biashara hiyo.

Alianzisha kioski hiyo hatua chache kutoka kituo hicho cha Naivasha ICD.

John Chege Wanjiku, ambaye ni mfanyabiashara wa mkahawa katika eneo hilo, pia analalamikia kupungua kwa biashara kufuatia kuhamishwa kwa shughuli za bandari hadi Mombasa.

“Kabla ya amri hiyo kutolewa nilikuwa nikivuna faida nzuri kutokana na biashara hii. Lakini tangu rais alipotoa amri hiyo, biashara imedorora kiasi kwamba natafakari kufunga,” akasema Bw Wanjiku.

Kwa upande mwingine biashara imeanza kuinuka Mombasa na vituo vya karibu.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya kuanza kula mahindi yaliyokuzwa kutumia mbinu ya GMO

Ruto, Raila kumenyania kiongozi wa wengi bungeni

T L