Wafanyikazi wasitisha mgomo Mombasa baada ya kulipwa

Wafanyikazi wasitisha mgomo Mombasa baada ya kulipwa

Na WINNIE ATIENO

GAVANA Hassan Joho jana Jumatatu alifanikiwa kushawishi baadhi ya wafanyikazi katika Kaunti ya Mombasa kurejea kazini, baada ya kuanza kuwalipa mishahara yao.

Hapo jana wafanyikazi wapatao 4,000 wa kaunti walianza mgomo baridi.

Hata hivyo, kufikia jana jioni, baadhi yao walianza kupokea mishahara na wakarejea kazini.

“Tunawataka wafanyikazi wawe watulivu kwa sababu Gavana Joho ametuhakikishia watu wataanza kulipwa mishahara yao. Bw Joho pia amesema tutapata bima ya afya,” alisema katibu wa muungano wa wafanyikazi wa serikali za kaunti, Haji Mwinyi Kibwana.

Bw Mwinyi alisema wafanyikazi anaowakilisha hawataendelea na mgomo huo, baada ya kufanya mazungumzo na serikali ya Kaunti ya Mombasa ulioongozwa na Gavana Joho.

Kulingana na Bw Mwinyi, wafanyikazi hao watasubiri wiki hii ili maafikiano yao yatekelezwe.

Awali, wafanyikazi hao walikuwa wametoa ilani ya mgomo wakilalamika kutolipwa mishahara yao.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Maafisa wa Matibabu (KUCO) tawi la Mombasa, Bw Frankline Makanga, alisema baadhi ya wafanyikazi katika idara ya afya wameanza kupokea mishahara yao.

Bw Makanga alisema watasitisha mgomo endapo wote watapokea mishahara yao.

  • Tags

You can share this post!

Mudavadi ayumba uchaguzi ukibisha

Vilio Koome aingilie kati kesi za kupinga ufufuzi wa Mumias

T L