Habari MsetoSiasa

Wafisadi wahukumiwe kifo – Wetangula

March 5th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

CHAMA cha Ford-Kenya kinataka watu wanaopatikana kushiriki ufisadi nchini kuhukumiwa kifo na mali yao kutwaliwa na serikali.

Kwenye mapendekezo kilichowasilisha kwa Jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI) jijini Nairobi jana, chama kilisema kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee, ambapo vita dhidi ya ufisadi vitazaa matunda.

Kiongozi wa chama hicho, Bw Moses Wetang’ula alisema kuwa ufisadi umegeuka kuwa mojawapo ya changamoto kuu zinazoikumba nchi kwa sasa.

“Wakenya wanateseka sana kutokana na madhara ya ufisadi. Ni wakati tuimarishe vita hivyo ili kuhakikisha kuwa wanaoadhibiwa wanakuwa mfano kwa wengine,” akasema Bw Wetang’ula, ambaye pia ni Seneta wa Kaunti ya Bungoma.

Alisema kuwa serikali imekosa kuifadhili Idara ya Mahakama ifaavyo, hali ambayo imeyumbisha vita dhidi ya janga hilo.

Alitoa mfano kuhusu kesi ya ufisadi katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ambapo washukiwa wakuu nchini Uingereza walihukumiwa baada ya kupatikana na hatia, huku kesi za wale washukiwa nchini zikiwa bado zinaendelea.

Aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Bw James Oswago na Bw Trevy Oyombra ndio walitajwa kuwa wahusika wakuu kwenye sakata hiyo iliyoibuika mnamo 2014.

Chama pia kiliunga mkono mfumo ambapo Rais na Naibu Rais wanachaguliwa moja kwa moja na wananchi.

Chini ya utaratibu huo, Rais atamteua Waziri Mkuu na manaibu wake wawili kutoka chama kilicho na idadi kubwa zaidi ya wabunge, ambapo baadaye wataidhinishwa na Bunge la Kitaifa.

Chama kilipendekeza utathmini wa kina wa baadhi ya tume za kikatiba, kikizitaja kuwa “mzigo mkubwa kwa mlipa ushuru.”

Baadhi ya tume kilichopendekeza zifutiliwe mbali ni Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA), Tume ya Kitaifa Kuhusu Usawa wa Kijinsia (NGEC) na Tume ya Kitaifa Kuhusu Huduma za Polisi (NPSC).

Na ili kulainisha utungaji wa sheria nchini, kinapendekeza Seneti kupandishwa hadhi, kama ilivyo katika baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kama Uingereza.

“Seneti inapaswa kutekeleza majukumu muhimu kama upigaji msasa wa maafisa wakuu wa serikali kama vile mabalozi, mawaziri, wakuu wa idara kati ya wengine kama ilivyo katika nchi zinazozingatia mfumo wa kidemokrasia,” akasema Bw Wetang’ula.

Ili kuharakisha mshikamano wa kikanda, kilipendekeza kuharakishwa kwa taratibu za uunganishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuondoa vikwazo vyote vya kisiasa na kiuchumi vilivyopo kwa sasa.

Pia kilipinga pendekezo la kubuniwa kwa majimbo, badala yake kilipendekeza miungano ya kiuchumi iliyopo kupewa nguvu na kutambuliwa kikatiba.