Habari Mseto

Wafu wakosa kuzikwa eneo la makaburi likigeuzwa uwanja wa kukuza nyasi za kuuza

January 1st, 2024 1 min read

Na RUTH MBULA

SERIKALI ya Kaunti ya Kisii inahangaishwa na suala la wafu ambao miili yao imekosa pa kuzikwa baada ya eneo la makaburi ya umma kudaiwa kunyakuliwa na kugeuzwa uwanja wa kukuza nyasi.

Kaunti hiyo inang’ang’ana kupata makaburi ya kuzika miili ambayo haijatwaliwa na ambayo kwa sasa inazidi kusongamana katika mochari mbalimbali za umma na za kibinafsi.

Miili hiyo ambayo haijatwaliwa ni ya watu waliokufa bila makazi rasmi au ardhi waliyorithi ambapo wangezikwa.

Suala hilo vilevile limeathiri jamii jirani zilizokuwa zikitegemea eneo la Makaburi ya Nyambera ambalo sasa limegeuzwa ardhi ya kibinafsi ya kukuza nyasi za kuwalisha mifugo.

Nyambera ilikuwa moja kati ya makaburi mjini Kisii ikifuatia na sehemu nyingine ya ardhi karibu na afisi ya aliyekuwa kamishna wa wilaya, iliyonyakuliwa katika miaka ya 1990 ambapo mabaki ya wafu yalifukuliwa na kutupwa na mabwenyenye wa kisiasa.

Eneo hilo la makaburi lililopo kwenye barabara kuu ya Kisii-Ogembo, mita chache kutoka Kisii Mwalimu Hotel ilinyakuliwa na watu wenye ushawishi kisiasa waliofukua wafu, wakatupa mabaki yao kwenye majaa ya taka kabla ya kugeuza ardhi hiyo kuwa mali ya kibiashara.

Gavana wa Kisii Simba Arati amesema wanajishughulisha kusaka kipande kingine cha ardhi kitakachotumika kama makaburi.

“Sasa wanaendesha kilimo kwenye Makaburi ya Nyambera baada ya kunyakua ardhi hiyo. Walifukua mabaki ya watu na kuteketeza mifupa ili kuandaa ardhi hiyo kwa kilimo,” alisema Gavana Arati.