Wafuasi wa Hasla wakosoa Rais ‘kudai amestawisha kilimo’

Wafuasi wa Hasla wakosoa Rais ‘kudai amestawisha kilimo’

Na BENSON MATHEKA

WASHIRIKA wa Naibu Rais William Ruto kutoka eneo la Mlima Kenya wanalaumu washauri wa Rais Uhuru Kenyatta wakidai wamempotosha kiongozi wa taifa kuhusu hali ya kilimo nchini.

Wanasiasa hao wakiwemo wabunge, magavana na maseneta walidai kwamba hotuba ya rais ya hali ya nchi kuhusu kilimo haikuwakilisha ukweli wa mambo.

Viongozi hao Anne Waiguru, wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Ndindi Nyoro (Kiharu), Alice Wahome (Kandara), Kimani Ichungwa (Kikuyu), Rahab Mukami (Nyeri), Susan Kihika (Nakuru), Faith Gitau (Nyandarua) na Irungu Kang’ata (Muranga) walisema washauri wa Rais Kenyatta walimpa ripoti ya uongo kuhusu ya sekta ya kilimo nchini.

Wakizungumza wakiwa katika Kaunti ya Nyeri mbele ya Dkt Ruto, viongozi hao walisema mapato ya wakulima yamepungua huku gharama ya mbolea ikipanda tofauti na ilivyodai ripoti ya Rais Kenyatta aliyotoa Jumanne wiki jana.

Walisema Rais Kenyatta anapaswa kupata ripoti ya hali halisi ya kilimo kutoka kwa wizara ya Kilimo ambayo inaeleza masaibu wanayopitia wakulima mashinani.

“Tunataka kumweleza Rais kwamba wakulima wanateseka. Anafaa kuwafuta kazi wnaompotosha kwa sababu alichoripoti bungeni ni tofauti na kile ambacho wakulima wa Kenya wanapitia mashinani,” alisema Bw Nyoro.

Aliongeza kuwa bei ya mbolea ambayo Rais Kenyatta alisema imeshuka imepanda hadi Sh5000 kwa gunia ilhali ilikuwa chini wakati wa serikali zilizotangulia.

Viongozi hao waliwataka maafisa wa serikali wanaosimamia kilimo kuacha kumdanganya Rais kwamba mambo yako shwari ilhali ukweli ni kuwa wakulima wanapitia wakati mgumu.

“Tunawaomba wakome kumpotosha Rais kwa sababu bei ya chai, kahawa na maziwa imeshuka na wakulima wanateseka sana,” alisema Bw Ichungwah.

Walisema kwamba wana imani kuwa Dkt Ruto atatatua shida za wakulima iwapo atashinda urais na kuunda serikali kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Bw Gachagua alisema kwamba masaibu ya wakulima wa chai, kahawa na maziwa yanafaa kushughulikiwa kwa kuwa wameteseka kwa muda mrefu.

Bw Ichungwa alisema kwamba nchi haiwezi kuweka sera mbaya na kwamba ufufuzi wa uchumi unapaswa kupatiwa kipaumbele.

Bi Waiguru alisema kwamba wakazi wa Mlima Kenya wamejiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwa sababu kina ajenda ya kubadilisha uchumi.

Akizungumza katika mikutano kadhaa ya kuvumisha ajenda yake ya hasla, Dkt Ruto alisema kwamba juhudi za UDA za kubadilisha uchumi haziwezi kuzuiwa na yeyote.

“Nitahakikisha kuwa tumetimiza ahadi ya kubuni nafasi za kazi kwa kuwekeza katika viwanda, makao na mipango ya kilimo,” alisema Dkt Ruto.

Alifichua kwamba atashirikiana na viongozi kutoka kote nchini kuimarisha UDA kiwe na nguvu na kubadilisha ajenda ya maendeleo ya nchi hii.

You can share this post!

Joho ampa Raila masharti makali

Shujaa yarejea nyumbani na majeraha Kabras ikikwamilia juu...

T L