Kimataifa

Wafuasi wa Tshisekedi na Kabila wazua taharuki DRC

July 23rd, 2019 2 min read

Na AFP

SERIKALI ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilitangaza Jumatatu marufuku ya mikutano ya kisiasa jijini Kinshasha wiki hii.

Hatua hiyo ni kutokana na taharuki inayoendelea kutanda kati ya wafuasi wa Rais Felix Tshisekedi na Rais Mstaafu Joseph Kabila.

Uhasama kati ya wafuasi wa viongozi hao wawili umezuka miezi sita pekee baada ya Rais Tshisekedi kuchaguliwa na kuapishwa kama kiongozi wa nchi huku mtangulizi wake Kabila akistaafu baada ya kuongoza taifa hilo kwa muda wa miongo miwili.

Taharuki kati ya wafuasi wa viongozi hao ilijitokeza Jumapili mjini Kinshasha baada ya kitengo cha vijana wa chama chake Rais Tshisekedi, Democracy and Social Progress(UDPS) kutangaza kwamba kitaandaa maandamano makubwa dhidi ya uwaniaji wa waziri wa zamani wa haki na katiba Alex Thambwe, anayelenga kutwaa urais wa bunge la seneti.

Kundi la Kabila nalo lilijitokeza kujibu lile la Rais Tshisekedi na kusema litaandamana ili kuunga uwaniaji wa Bw Thambwe, ambaye ni mwandani wa rais huyo wa zamani.

Mkuu wa Polisi mjini Kinshasa, Jenerali Sylvano Kasongo kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja katika runiga ya serikali alisema kwamba gavana wa mji huo amepiga marufuku mikutano yote ya kisiasa wiki hii kutokana na kuzidi kwa uhasama kati ya wafuasi wa viongozi hao wawili.

“Gavana amewataka maafisa wa usalama kuweka mikakati yote ya kiusalama. Mtu yeyote atakayedhubutu kuandamana au kuvuruga amani atakabiliwa vikali na polisi,” akasema Jenerali Kasongo.

Viongozi wa zamani

Akizungumza na wanahabari, msemaji wa kitengo cha vijana wa UDPS, Fils Mukoko naye alisema walipanga kuandamana ili kupinga uwepo wa viongozi wa zamani kwenye asasi za serikali.

Chama cha Bw Kabila cha FCC kilishinda viti vingi kwenye seneti na mabunge ya mikoa, huku washirika wake pia wakishinda viti vingi vya ugavana.

Kati ya wawaniaji walioorodheshwa kuwania viti muhimu saba kwenye bunge la seneti, hakuna hata moja anayetoka katika chama cha Rais Tshisekedi cha CACH licha ya chama hicho kuingia kwenye makubaliano ya kufanya kazi pamoja na FCC baada ya uchaguzi mkuu.

Miezi sita baada ya Rais Tshisekedi kuapishwa na mwezi mmoja tangu kuteuliwa kwa Waziri Mkuu, Ilunga Ilunkamba ambaye alipendekezwa na Bw Kabila, viongozi wa vyama vya CACH na FCC bado wanaendelea kushauriana na hawajaafikiana kuhusu mfumo wa kugawa nafasi za wizara serikalini.