Habari MsetoSiasa

Wafugaji kuzuia mawakili wa Moi kutwaa ng'ombe

July 2nd, 2019 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

KUNDI la wafugaji kutoka Kaunti ya Samburu limefika kortini likitaka kusimamisha mpango wa kuuza mifugo yao ili kulipa deni la Sh8.2 milioni wanalodaiwa na mawakili wa Rais mstaafu Daniel Moi.

Wafugaji hao walifika katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Nyeri kupitia mwakilishi wao Richard Leiyagu, kwa ombi la dharura kuwa korti lisitishe hatua hiyo.

Bw Leiyagu alisema tayari wamepokea barua kutoka kwa kampuni ya upigaji mnada ya Nasiok Auctioneers, ambayo inataka ng’ombe 1,300, vyombo vya nyumbani na magari.

Kampuni hiyo iliagizwa na kampuni ya mawakili ya Kiplenge & Kurgat Advocates, ambao walimwakilisha Mzee Moi katika kesi hiyo iliyodumu miaka minane, kuhusu umiliki wa ardhi ya ekari 17,105, eneo la Laikipia Kaskazini.

Wakazi 248 wa jamii hiyo walikuwa wamemshtaki Mzee Moi kuwa alipatia Shirika la Kulinda Wanyama Pori (KWS) shamba lao.

Mawakili wa Moi walifika kortini mara 107 kutoka Machi 15, 2010 hadi Julai 24, 2017, wakati Jaji Lucy Waithaka alipotupilia mbali dai la wakazi hao kuwa ardhi husika ni yao.

Mawakili wa Moi walikuwa wakitaka kulipwa Sh40 milioni na wafugaji hao kama gharama ya kesi lakini naibu msajili wa Mahakama Kuu, Demacline Bosibori akaagize walipe Sh8 milioni.

Wafugaji hao wanasema mifugo yao ikipigwa mnada watabaki bila chochote cha kujikimu kimaisha.