Habari Mseto

Wafugaji wa kuku Kiambu wanunuliwa kiangulio

March 29th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAFUGAJI wa kuku wa Kiambu Poultry Farmers Society wamejitolea kupiga hatua katika mradi huo.

Mbunge wa Thika, mhandisi Patrick’Jungle’ Wainaina, na mwenzake wa Gatundu Kaskazini, Bi Wanjiku Kibe, walitoa hamashisho la kuwasaidia wafugaji hao ili wajiendeleze kutokana na biashara hiyo.

Wafugaji hao wapatao 500 walikongamana eneo la Ngoingwa, Thika, mnamo Alhamisi kwa lengo la kuhamashishwa jinsi ya kujiendeleza hasa kupitia ufugaji wa kuku.

Bw Wainaina aliwafadhili na  mtambo uliyogharimu Sh 1 milioni na lina uwezo wa kuangua vifaranga 1,200 kwa wakati moja huku pia wakikabithiwa chakula cha kuku cha magunia 40.

“Mimi nataka kuona mfugaji wa kuku akinufaika pakubwa na huo mradi, na hilo litawezekana tu iwapo mtashikana pamoja kuwa kitu kimoja,” alisema Bw Wainaina.

Aliwahimiza kuzingatia ajenda nne za serikali hasa maswala ya ajira,  na ujenzi wa nyumba.

Alisema shida kubwa inayoshuhudiwa na wafugaji wa kuku hapa nchini ni kuwa nchi jirani zimemwaga bidha zao kama mayai hapa nchini na kusababisha “wafugaji wetu kuuza bidhaa zao kwa bei duni.”

“Mimi kama kiongozi wenu nitahakikisha mumepata soko. Pia nitafanya juhudi kuona ya kwamba kuna kichinjio cha kuku hao,” alisema Bw Wainaina.

Kati ya wafugaji wa kuku walio Kaunti ya Kiambu, 800 wanafuga aina ya kuku wa layers. 400 ni wale wa Broillers na 200 ni wa kienyeji.

Hao ni wale wamepata vyeti maalum vya kutambulika rasmi.

Kujiamini

Bi Kibe ambaye ni Mbunge wa Gatundu Kaskazini aliwahimiza wafugaji hao kujiamini na kufanya kazi hiyo kwa bidii.

“Iwapo mtaungana kwa pamoja mtafika mbali na biashara yenu. Kwa hivyo kuweni pamoja  na muwe na maono,” alisema Bi Kibe.

Alisema atashirikiana pamoja na Bw Wainaina ili kuona ya kwamba wafugaji hao wananufaika.

Mwenyekiti wa wafugaji hao Bw Zachary Waweru Munyambu, alisema kwa muda mrefu wafugaji wa kuku kutoka Kiambu wamepitia masaibu mengi na huu ni wakati mwafaka wa kupata usaidizi.

Bi Elizabeth Wamuyu, mfugaji wa kuku za kienyeji alitoa mwito kwa viongozi hao wawili wafanye juhudi kuona ya kwamba wafugaji hao wamehamasishwa vilivyo.

“Tungetaka kupewa mikopo pia kama wafugaji ili tuweze kujiendeleza zaidi,” alisema Bi Wamuyu.

Bw John Mwaniki, mfugaji wa kuku wa mayai alisema kuku wapatao 500 hula kilo 70 za chakula kila siku na gunia moja la chakula cha kuku ni Sh 2,500.

Baadhi ya  wafugaji hao walitoka sehemu za Gatundu Kaskazini, Juja, Ruiru, na Thika.