Habari Mseto

Wafugaji wa kuku waiomba serikali kuingilia kati kupunguza gharama ya lishe

August 17th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KWA karibu miaka mitano mfululizo, sekta ya ufugaji wa kuku nchini imekuwa ikipitia changamoto chungu nzima hasa kwa sababu ya kuku wa nyama na mayai kutoka mataifa jirani kuruhusiwa kuingia.

Wafugaji wanadai mazao ya nje ni ya bei ya chini, suala linalowalazimu kuuza yao kwa bei ya chini pia.

Hili linachangiwa na kutokuwepo kwa sheria maalum kudhibiti bei ya kuku na mayai, yanayoingia Kenya.

Wafugaji wanalalamika kwamba wakikokotoa hesabu ya mapato na gharama waliyotumia kuzalisha mazao ya kuku, wanachopata ni hasara.

“Ufugaji wa kuku Kenya unaendelea kufifia, sababu ikiwa kuku na mayai yanayotoka nje yameharibu soko. Sisi wakulima hatuna budi ila kushusha bei ya mazao yetu ili tupate wateja. Ikumbukwe gharama ya chakula cha mifugo inaendelea kukwea mlima,” anateta mfugaji wa kuku wa mayai Bw Wilson Mwangi.

Vifaranga hula chakula maalum aina ya chick mash ambapo gunia la kilo 70 linauzwa Sh2,700. Wanaoendelea kukua, growers, hula growers mash gunia likigharimu Sh2, 200, huku la walioanza kutaga, layers likiuzwa Sh2, 350.

Kulingana na mfugaji Caroline Murigu, wa Kaunti ya Kiambu, anasema mawakala pia wamechangia kudorora kwa bei.

“Soko la mazao ya kuku limejaa mawakala ambao ni wa humuhumu nchini. Wanaendea kuku na mayai nje kwa bei ya chini, na ili kupata faida ya haraka lazima wauze kwa bei ya chini kuliko yetu,” Caroline anaeleza.

Kulingana na mfugaji huyu, suala la kupanda kwa gharama ya uzalishaji likiunganishwa na kero la mawakala, mkulima hatakuwa na budi ila kupata hasara inayotishia kuacha ufugaji wa kuku.

“Sekta ya kuku Kenya itaimarika gharama ya chakula cha mifugo ikishushwa, pamoja na kudhibiti mawakala,” anapendekeza Caroline.

Kreti ya mayai yasiyoanguliwa kwa sasa inauzwa chini ya Sh300 ikilinganishwa na miaka ya awali ambapo ilikuwa hata zaidi ya Sh350.

Mayai yanayoanguliwa vifaranga, maarufu kama ya jogoo, kreti moja inauzwa chini ya Sh550.

Vichinjio vinauza kuku mmoja aina ya broiler chini ya Sh450, wa kienyeji wa kisasa au aliyeboreshwa akiuzwa Sh550.

Hii ina maana kuwa mfugaji amenunuliwa kwa bei ya chini.

Miaka ya awali, broiler aliuzwa hata zaidi ya Sh500, kuku wa kienyeji wa kisasa Sh700.

Aidha, bunge linapaswa kupitisha sheria zitakazodhibiti uingiaji wa kuku na mayai nchini, ambapo mazao hayo yanafaa kutozwa ushuru ili kusawazisha na yanayozalishwa Kenya.

Mkurugenzi mkuu wa watengenezaji wa chakula cha mifugo na kuku nchini (Akefema), Dkt Humphrey Mbugua hata hivyo, anahimiza wakulima kujiundia chakula wenyewe ili kupunguza gharama.

“Gharama inayowakodolea macho itapunguzwa wakijiundia chakula, na ambacho wana uhakika wa madini yake,” anasema Dkt Mbugua.

Kulingana na mdau huyu ni kwamba hili linaweza kuafikiwa wafugaji wakiungana kwa makundi.

“Makundi yatakusanya pesa, wajiundie chakula na hata kutengeneza kiwanda cha chakula cha mifugo watakachojiuzia kwa bei nafuu na wateja wengine,” anaeleza mtaalamu huyu.

Kiambu Poultry Society, ni chama cha ushirika ambacho wafugaji kadhaa wameungana na kujiundia chakula cha mifugo.

“Mbali na kupunguza gharama, muungano wetu unaturahisishia kupata soko la mazao,” anasema mwanachama Zachary Munyambu ambaye pia ni mfugaji.

Bw Munyambu anasema Kiambu Poultry Society pia hupata oda ya kuku na mayai katika hoteli na taasisi mbalimbali nchini.

Ili kuepuka kikwazo cha bei duni ya mayai, Margaret Maina, mfugaji Kiambu, huangua vifaranga kwa viangulio.

“Yai moja bei ya rejareja linanunuliwa chini ya Sh20, nikiliangua kifaranga wa siku moja ninamuuza zaidi ya Sh80. Ninapendekeza kuongeza mazao thamani,” asema Bi Maina.

Mfugaji chipukizi anahimizwa kupata mafunzo kama vile ya namna ya kupokea vifaranga, kuwatunza, lishe, maji, usafi na matibabu. Baadhi ya wafugaji wameishia kupata hasara isiyomithilika kwa ajili ya kutokuwa na maarifa kulea kuku. Mafunzo pia yatamnoa jinsi ya kupata soko la mazao.