Wafugaji wapinga New-KCC kubinafsishwa

Wafugaji wapinga New-KCC kubinafsishwa

NA STANLEY KIMUGE

BAADHI ya wafugaji wamepinga mipango ya serikali kubinafsisha shirika la maziwa la New KCC, wakionya kuwa hatua hiyo haifai na itawaumiza.

Badala yake, wanataka umiliki wa shirika hilo kwanza urejeshewe wakulima kabla ya uwepo wa mazungumzo yoyote kuhusu ubinafsishaji wake.

Mnamo 2019, Baraza la Mawaziri lilisimamisha mipango ya kubinafsisha shirika hilo, likieleza hofu kuhusu hatua ya kuliacha mikononi mwa wawekezaji wa kibinafsi.

Mnamo 2015, serikali ililitengea shirika hilo Sh400 milioni ili kuisaidia kuanza kiwanda cha kutengeneza maziwa ya unga mjini Eldoret. Shirika hilo pia limekuwa likipanua viwanda vyake vya Nyahururu na Dandora.

Hapo awali, serikali ya NARC ilichukua udhibiti wa shirika hilo na kuanza kutafuta mnunuzi baada ya kuchukua uongozi mnamo 2003 kutokana na usimamizi mbaya.

Utawala wa Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki ulilipa deni la Sh547 milioni ambazo shirika hilo lilikuwa likidaiwa, ikiahidi kurejesha usimamizi wake mikononi mwa wakulima baada ya hali yake kuimarika.

Baadhi ya wakulima wasema shirika hilo limesaidia sana kuboresha bei ya maziwa kwa kununua maziwa mengi na kuyageuza kuwa maziwa ya unga.

“Kulingana na ahadi ya serikali ya kuanzisha bei ya wastani ya kununua maziwa, tunahofia kuwa hatua yoyote ya kubinafsisha shirika hilo itawaathiri sana wakulima kwa kuwaacha mikononi mwa wawekezaji wa kibinafsi,” akasema Bw David Kipchumba, ambaye ni mfugaji katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Mkurugenzi wa Chama cha Kitaifa cha Wakulima Kenya (KFA), Kipkorir Menjo, alisema kuwa lazima usimamizi wa shirika hilo urejeshewe wafugaji.

Alisema kuwa wao ndio wamiliki wakuu, hivyo ndio wanafaa kuamua kuhusu ikiwa shirika linafaa kubinafsishwa au la.

“Naamini kuwa hisa na faida ambazo shirika hilo lilipata zinaweza kutumika kulipia madeni yoyote linayoweza kuwa nayo,” akasema.

Bw Henry Otyula, ambaye ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kaunti ya Bungoma, alisema kuwa wafugaji wengi wako gizani kuhusu umiliki halisi wa shirika hilo.

  • Tags

You can share this post!

Barcelona wakomoa Sevilla na kufungua mwanya wa alama nane...

Lengo la Murang’a Seal ni kusaidia vijana kutimiza ndoto...

T L