Habari Mseto

Wafungwa 39 waachiliwa kupunguza msongamano magerezani

March 28th, 2020 1 min read

PHILIP MUYANGA NA FAUSTINE NGILA

Wafungwa 39 Jumamosi wameachiliwa kutoka jela za Mombasa katika mpango wa Idara ya Magereza wa kupunguza msongamano.

Wafungwa hao walikuwa wanatumikia kifungo cha chini ya miaka mitatu.

‘”Orodha ya wafungwa itaendelea kusasishwa mara kwa mara na kulingana na maamuzi ya mahakimu walioamua kesi zao,” alisema naibu msajili wa mahakama ya Mombasa Bi Christine Ogweno.

Kulingana na Bi Ogweno, mchakato huo bado  unaendelea na utafuata faili za kesi kutoka korti ya Shanzu na ile ya Kwale.

Wakati huo huo, hakimu mkuu wa Mombasa Edna Nyaloti na Bi Ogweno walikuwa wanatakiwa kuangalia upya bondi na dhamama wanaopewa washukiwa ili kupunguza msongamano magerezani.

Shughuli hiyo inatarajiwa kufanyika kupitia video ya moja kwa moja mtandaoni ili ilikuzuia kuenea kwa virusi vya corona.