Habari MsetoSiasa

Wafungwa wamlilia Rais awaachilie

March 31st, 2019 1 min read

BENSON MATHEKA NA KNA

WAFUNGWA ambao wamehudumu vifungo kwa miaka mingi katika gereza la Kericho, wamemuomba Rais Uhuru Kenyatta kutumia nguvu zake za kisheria kuwahurumia na kuwaachilia huru.

Bw Robinson Ogembo, 51, ambaye alifungwa kwa kutekeleza mauaji na ambaye amekuwa jela miaka 21, alimuomba Rais kuachilia baadhi yao ambao tayari wamehudumu vifungo kwa miaka mingi.

Ogembo ambaye alipewa fursa kuzungumza mbele ya kamati msamaha ya Rais (POMAC), alimshukuru Rais kwa kuteua jopo hilo kuangazia maslahi ya wafungwa kwa lengo la kuachilia baadhi yao.

Kamati hiyo iko katika harakati za kuzunguka magereza yote nchini kupokea maoni na maombi kutoka kwa wafungwa. Ilikuwa ikiongozwa na naibu mwenyekiti Dkt Janet Kirui ilipotembelea Kericho.

Baada ya kupokea maombi, kamati itasikiza, kufanya mahojiano, uchunguzi, utafiti na ikusanye habari huku ikiwaelimisha wafungwa jinsi ya kutafuta msamaha wa Rais na kuachiliwa.

Dkt Kirui alisema wafungwa ambao wamehudumu zaidi ya thuluthi moja ya kifungo walichopewa wako huru kutafuta msamaha wa Rais.

Alisema hata watu ambao walikosewa na wale walioko jela watatafutwa na kuhojiwa kabla ya wafungwa kuachiliwa.

Kisheria, Rais ana mamlaka ya kusamehe wafungwa ambao kamati itathibitisha wamebadilika baada ya kuhudumu kwa miaka mingi gerezani.

Hata hivyo, kabla ya kutoa msamaha huo ni lazima usalama wa mfungwa uhakikishwe akitoka jela miongoni mwa mambo mengine.