Na PHILIP MUYANGA
WAFUNGWA wanne wameishtaki Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wakitaka kukubaliwa kupigia kura magavana, maseneta, wabunge, madiwani na wabunge wawakilishi wa wanawake katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika ombi lao kwa Mahakama Kuu ya Mombasa, Douglas Onyango, Edwin Njuguna, Samuel Mwaghania na Haron Mberia wanataka agizo litolewe kwa mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati ili wakubaliwe kupiga kura sawa na wananchi wengine.
Kulingana nao, kutokana na kuwa walikubaliwa kushiriki katika kura ya maamuzi 2010 na uchaguzi wa 2013 na 2017 wa urais, hakuna sababu kuwanyima haki ya kuchagua viongozi wengine watano wa kisiasa.
“Tunahisi tulibaguliwa na maamuzi ya IEBC kwa kutukataza kupigia kura gavana, seneta, mbunge, mwakilishi wa wanawake bungeni na diwani katika chaguzi za 2013 na 2017,” wakasema katika ombi lao.
Walalamishi hao ambao wamemshtaki pia Mwanasheria Mkuu wanasema hakuna sababu ya kuwanyima haki ya kuchagua wagombeaji wa viti hivyo ambao wanaamini wana uwezo wa kutoa huduma bora kwa wafungwa.
Walizidi kusema kuwa, wakinyimwa nafasi ya kupiga kura, itakuwa sawa na kuwanyima nafasi ya kujiendeleza kikamilifu kama binadamu na hilo litakuwa ni ukiukaji wa Katiba.