Habari Mseto

Waganga wa kienyeji wataka serikali iwatambue kwa kutibu magonjwa

May 28th, 2024 1 min read

NA MAUREEN ONGALA

WAGANGA wa kienyeji katika eneobunge la Magarini, Kaunti ya Kilifi, wametoa wito kwa serikali ya kitaifa pamoja na ile ya kaunti kuwatambua kutokana na juhudi zao za kutoa matibabu ya maradhi mbalimbali katika jamii.

Wakiongozwa na msimamizi wa kituo cha utamaduni cha Magarini, Bw Tusma Nzai, walisema matibabu ya kienyeji yamesaidia wagonjwa hasa katika jamii ya Mijikenda tangu enzi za jadi.

“Tunaomba Serikali ya Kaunti na Serikali ya Kitaifa waweze kuja chini na kushirikiana na waganga pamoja na madaktari ili tutoe suluhu ya kuokoa maisha,” akasema.

Bw Shungu Thuva, mganga katika kituo hicho, alisema wangependa kuhusishwa katika utafiti wa tiba za kiasili za maradhi sugu nchini.
Daktari mkuu wa maradhi ya kifafa Kaunti ya Kilifi, Bw Eddie Chengo, aliunga mkono kauli hiyo akisema waganga wamekuwa na mchango mkubwa katika jamii na hivyo wanapaswa kupewa fursa ya kuonyesha baadhi ya dawa wanazotumia, kwani huenda ikasaidia shughuli za matibabu hospitalini.

“Huwezi kuwapuzia, huwezi kupita nyumba kumi kabla hujapata mtabibu mmoja na kwa hivyo ni lazima tuwape hamasa ya kutosha ili kuwa na uwezo wa kutibu ama kudhibiti magonjwa katika uwezo wao,” akasema.

Jamii ya Mijikenda eneo la Pwani huthamini Kaya na kuendelea kuhifadhi misitu hiyo ya kiasilia ambayo mbali na kuwa sehemu takatifu za kufanyia maombi na tambiko zao, miti hiyo hutumika kama dawa ya kienyeji.