Waganga waonywa dhidi ya kutibu wasichokielewa

Waganga waonywa dhidi ya kutibu wasichokielewa

NA KALUME KAZUNGU

MUUNGANO wa kitaifa wa waganga wa mitishamba (NATHEPA), tawi la Lamu, limehimiza wanachama wake waelimishwe dhidi ya kutibu maradhi ambayo si ya kiwango chao.

Muungano huo umeiomba serikali kupitia wizara ya afya kuandaa kongamano ambalo litasaidia kuwahamasisha.

Mwenyekiti wake, Bw Ali Salim, alielezea hofu kwamba baadhi ya wanachama wake wamekuwa wakidai wana uwezo wa kuwatibu wagonjwa wa maradhi kama vile Ukimwi, Covid-19, polio na mengineyo, hali ambayo ni hatari.

Bw Salim alikiri kuwa waganga wengi hukumbwa na kipindi kigumu kutambua maradhi yasiyo ya kiwango chao kwa kuwa hawana njia za kubaini au kutambua dalili za maradhi hayo.

“Zamani tulikuwa hatuna la kuhofia kwani hakukuwa na maradhi ya kiajabu kama dunia ya leo. Kwa sasa kumechipuka maradhi, ikiwemo Ukimwi, polio na Covid-19. Maradhi haya ni vigumu kuyashughulikia,’ akasema.

Pia alihofia kuwa katika harakati za kutibu kile wasichokielewa, baadhi yao huenda wakaambukizwa hasa ikiwa ni maradhi ya kuambukiza.

Waganga hao pia wanaomba serikali iwasaidie kwa vifaa vya kujikinga wanapookuwa kazini sawa na madaktari hospitalini.

“Ningeisihi serikali kutambua sekta hii muhimu ya waganga. Watupe barakoa, glovu na hata magwanda maalum ili tujikinge tunaposhughulikia wagonjwa wetu ili tusiambukizwe,” akasema Bw Mohamed mmoja wa wanachama wa muungano.

Wakazi hasa wale wa visiwa vya mbali na wa msitu wa Boni hutegemea sana huduma za madaktari wa mitishamba kutokana na hali mbovu ya miundomsingi.

You can share this post!

Serikali italipa fidia ya Sh14 bilioni kwa walioshambuliwa...

Brazil na Ivory Coast kuumiza nyasi leo